Nairobi, Kenya. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis amesema kwamba kesho akiwa Kenya atatoa ujumbe wa amani.
Kiongozi huyo Katika taarifa aliyoituma juzi, alitoa wito kwa waandaaji wa ziara yake wakumbuke kuomba ili ziara hiyo ilete matumaini kila mmoja.
Utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrak mwishoni mwa wiki ulionyesha kuwa asilimia 93 ya raia wa Kenya wana hamu ya ziara ya kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ulimwenguni.
“Wakenya wengi wanatarajia kujitokeza mapokezi ziara ya Papa kesho. Matarajio hayo yako kwa Wakenya wote bila kujali dini wala kabila,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Infotrak Angela Ambitho.
Alisema raia wa nchi hiyo 777 walihusishwa katika utafiti huo uliofanywa Ijumaa. Asilimia 98 ya Wakatoliki wanafurahia ziara ya Papa Francis na asilimia 91 ya Wakenya wa madhehebu na dini zingine walisema wanamkaribisha Kenya.
Utafiti huo ulionyesha kuwa Papa Francis anayefanya ziara yake ya kwanza Afrika anapendwa na Wakenya wote Wakatoliki na wasio Wakatoliki.
“Papa Francis anapendwa na Wakatoliki ambao wamekumbatia unyenyekevu wake na wito wa kushirikisha wote,” alisema Ambitho.
“Kupendwa kwa Papa kunaonekana kupiku Kanisa Katoliki ambalo licha ya kukumbwa na kashfa mbalimbali ulimwenguni lina wafuasi wengi Kenya,” aliongeza
Mabadiliko
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 95 ya Wakatoliki nchini Kenya wanahisi Papa Francis ataleta mabadiliko katika kanisa hilo.
Aidha, asilimia 98 ya Wakatoliki Kenya wanahisi kwamba Papa Francis ataleta mabadiliko mazuri katika dini ya Kikristo, asilimia 85 ya Wakenya wa madhehebu mengine wanahisi kwamba ataleta mabadiliko katika dini.
Alisema kuhusu hali ya uongozi ulimwenguni, asilimia 97 ya Wakatoliki Kenya wanahisi kwamba Papa Francis ataleta mabadiliko.
Pia, utafiti huo uligundua kuwa tangu achaguliwe kuongoza kanisa hilo ulimwenguni, asilimia 79 ya Wakenya walianza kujali familia zao zaidi na kuwaonea huruma wenzao.
Alisema matokeo ya utafiti huo si tofauti na uliofanywa kabla ya ziara ya Papa Francis katika mataifa ya Amerika Kusini, wengi walionyesha kupendezwa na sera zake.
Pia, baadhi ya maaskofu wa Kanisa hilo nchini Tanzania wanatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika ibada hiyo kwenye nchi za Kenya na Uganda.
Ziara hiyo ni ya kwanza Afrika kwa Papa Francis tangu ateuliwe kuwa kiongozi wa takriban Wakatoliki bilioni 1.2 duniani, mwaka 2013.
Taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba, ambazo ziliandikwa na gazeti moja la kila siku aliwataja maaskofu hao watakaoiwakilisha Tanzania katika ziara hiyo kuwa ni Desiderius Rwoma wa Bukoba, Liberatus Sangu wa Shinyanga na Paul Ruzoka wa Tabora.
Padri Saba alisema kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyotolewa katika mtandao wa Catholic News Service mapema mwezi huu, Papa Francis atawasili Kenya kesho.
Ratiba kiongozi huyo wa kanisa Katoliki akiwa Uganda inaonyesha, atatoa heshima kwa ajili ya kumbukumbu ya Waanglikana 23 na Mashahidi wa Kikatoliki 22, waliouawa kutokana na imani zao kwa amri ya Mfalme Mwanga II kati ya mwaka 1885 na 1887.
Novemba 28, mwaka huu atatembelea makaburi ya mashahidi wa Anglikana na Katoliki katika eneo la Namugongo ambako ataongoza ibada kwa ajili ya mashahidi hao jirani na makaburi ya Wakatoliki.
Kila ifikapo Juni 3 kila mwaka kuna mahujaji wanatembelea makaburi hayo na huita ni siku ya Mashahidi hao.
Baada ya kumaliza ziara kwenye nchi za Kenya na Uganda Papa Francis atakwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).Ziara hiyo ya Papa Francis ni muhimu hasa katika kipindi hiki kutokana na uhasama unaoendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya waumini wa Kiislamu na Kikristo pamoja na mashambulizi ya kigaidi Kenya.
Hii ni ziara ya kwanza ya Papa barani Afrika, tangu alipoingia madarakani.
Baadhi ya barabara ambazo atapita kwenye nchi za Uganda na Kenya zimewekwa lami huku ukarabati ukiendelea kuhakikisha maji hayasimami kwenye mitaro ya barabara.
0 comments:
Post a Comment