Katiba
ya mwaka 1977 inamtaka Rais kumteua waziri mkuu ndani ya siku 14 tangu
alipoapishwa na kulipeleka jina lake bungeni, lakini katiba hiyo ipo
kimya kuhusu uteuzi wa mawaziri, hivyo Rais anaweza kutumia muda wowote.
Wakati
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995 aliteua
baraza la mawaziri Novemba 28, siku tano baada ya kuapishwa, Jakaya
Kikwete alitangaza Baraza la kwanza Siku 14 baada ya kuapishwa na Dk
Magufuli hadi sasa, siku 25 zimepita tangu aapishwe Novemba 5, mwaka huu
hajafanya hivyo.
Kazi
ambazo Rais Magufuli ameanza kuzifanya bila mawaziri ni kuzuia safari
za nje, kuzuia sherehe za Uhuru na kuanza kupambana na wabadhirifu wa
fedha za umma.
Wasomi
hao wakilinganisha alichokisema kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa
Bunge, walisema kuwa ana njozi za Tanzania aitakayo huku akieleza wazi
kuwa anatambua kuna mawaziri, wabunge wanakula rushwa na akibainisha
wazi hana imani kama waliomo ndani ya CCM wanakula pia.
Mhadhiri
kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Elijah Kondi, alisema kuwa sababu za Magufuli kuchelewa kutaja Baraza la
Mawaziri ikilinganishwa na Serikali zilizopita inatokana na utendaji wa
Mawaziri wa Serikali iliyopita, wengi hawakufanya vizuri na baadhi yao
hata ushindi wao wa ubunge una maswali mengi.
Alisema
tayari ana njozi za anachotaka kukifanya, anapata wakati mgumu wa ni
nani mtu sahihi wa kumsaidia kutimiza njozi zake, hata ndani ya CCM
baadhi yao hawaaminiki na amekuwa akisema hivyo mara nyingi.
Alipozungumzia rushwa pia hakusita kuwahusisha walio ndani ya CCM, japo
siyo moja kwa moja.
“Inawezekana
waliopo wengi anaona hawawezi kuendana na kasi yake, pengine hata wale
anaoona wana afadhali walishawahi kupata kashfa mbalimbali, huku yeye
akiwa na njozi za kuanza upya na watu wenye utashi wa mabadiliko ya
kweli na ya wote, ”alisema Kondi.
Profesa
George Shumbusho, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema Rais
anapata wakati mgumu kuteua mawaziri kutokana na changamoto alizozitaja
siku ya kuzindua Bunge kuwa nyingi na nzito, zinazohitaji watu makini
kuzitekeleza.
Alisema
analazimika kufanya upembuzi yakinifu kujua ni nani na atashughulikia
eneo gani kama anavyotaka yeye, liendane na kasi na utendaji wake.
“Ninachokiona
anataka kuunda baraza makini hataki kurudi na kuhoji utekelezaji wa
kazi, kingine anahitaji aunde litakalokaa muda mrefu na kufanya
utekelezaji badala ya kuunda lingine kwa muda mfupi, ”alisema Profesa
Shumbusho.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhadhiri mwandamizi ambaye ni Mkuu wa
Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT),
Emmanuel Mallya, alisema anachukua muda kutaja Baraza la Mawaziri
kutokana na kutaka litakalotambua anataka nini kifanyike katika Serikali
yake ambayo amekuwa akiitaja moja kwa moja kuwa ya Magufuli.
Alifafanua
kuwa hataki kukurupuka na kujilaumu baadaye kutokana na utendaji
usioridhisha unaoweza kujitokeza asipokuwa makini, ndiyo maana anachukua
muda na kujaribu kuonyesha ni jinsi gani inawezekana kusimamia vitu na
vikaenda.
“Kwa
kuangalia kasi yake, unaona kabisa anapata wakati mgumu kupata viongozi
watakaofanya kazi kwa lengo moja ya mageuzi na mabadiliko, ndiyo maana
anachukua muda ili akija nalo liwe makini, ” alisema Mallya.
Mhadhiri
wa Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard
Mbunda, alisema kwenye mitandao ya kijamii kuna utani unazunguka kuwa
kwa kasi yake anaweza kufanya kazi hata bila kuwa na mawaziri.
“Ni
utani, lakini ukiuchunguza mara mbili unaona kabisa hata wananchi
wameona anachokifanya na wanahitaji kukiona hicho kutoka kwenye Baraza
lake,” alisema.
Alisema
kasi yake na kubana matumizi alikoanza nako anahitaji kuwa makini kwa
sababu alitamka anataka kuwa na baraza dogo la mawaziri.
Alifafanua
kuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2005, mawaziri na naibu wao
idadi yao ilikaribia 60, wakitumia mashangingi yanayokula mafuta, posho,
hivyo ili kudhibiti hilo atachukua muda pia, ikiwamo kuvunja baadhi ya
wizara kama ataona itafaa na kumsaidia anachotaka kukifanya.
CHANZO : MWANANCHI
CHANZO : MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment