MAMLAKA
ya Mapato Tanzania (TRA) imezuia kampuni ya Said Salim Bakhresa &
Co. Limited kupeleka makontena yake katika Bandari yake Kavu (ICD),
baada ya kugundulika kuwa baadhi ya makontena yalipitishwa bila kulipiwa
kodi.Kwa
mujibu wa barua ya TRA ya Novemba 17, mwaka huu, iliyosainiwa na
Wolfagang Salia kwa niaba ya Kamishina wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
kampuni hiyo imezuiwa kutumia bandari yake hiyo- Namba 03 hadi kesi hiyo
inayoshughulikiwa na mamlaka hiyo itakapotatuliwa.
“Unafahamu
kwamba uondoaji wa bidhaa kutoka eneo linalodhibitiwa na forodha,
ambalo kodi na ushuru wa serikali haujalipwa ni kinyume na sheria kwa
mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha
ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile husababisha upotevu wa mapato ya
Serikali.
“Kwa
sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia kupeleka makontena katika bandari yako
kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi suala hili litakapotatuliwa.
Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.
“Kutokana
na sababu hizo, tunasimamisha upelekaji wa makontena katika bandari
yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja. Hata hivyo utoaji wa bidhaa
zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,” ilisema taarifa hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo, alipoulizwa
alikiri mamlaka hiyo kumwandikia barua mfanyabiashara huyo huku
akisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa sababu
lipo katika uchunguzi.
“Ni
kweli barua ile ni ya kwetu, lakini mambo mengine bado yapo kwenye
uchunguzi, huyo (Bakhersa) ni kati ya wengine ambao tunaendelea
kuwafanyia kazi na tukikamilisha tutawajulisha” alisema Kayombo.
Kova kutoa tamko leo
Gazeti
hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova, ili kujua watu ambao wamekamatwa kutokana na
agizo la Rais Magufuli, alisema taarifa alizonazo bado hazijakamilika.
“Leo
sina chochote cha kusema bwana, kesho (leo) nitatoa taarifa kwa vyombo
vya habari ambayo ndiyo itakayofafanua kila kitu,” alisema Kova.
Alipofanya
ziara ya ghafla katika bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, aliwasimamisha kazi baadhi ya vigogo waliohusishwa na upotevu
wa makontena 349 ambayo yameisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80
kutokana na ukwepaji kodi na kuagiza wengine wakamatwe.
Taarifa ambazo gazeti hili imezipata, tayari maofisa kadhaa wa Bandari na wale wa TRA wamekamatwa kwa mahojiano zaidi.
Wahusika hao wanaendelea kushikiliwa na polisi huku uchunguzi wa akaunti zao pamoja na mali wanazomiliki ukifanywa.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa, maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), wameshaanza kuhakiki mali za maofisa kadhaa wa
mamlaka hizo.
Kutokana
na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,
Advera Bulimba, ambaye alisema kwa sasa bado wako kwenye uchunguzi wa
watuhumiwa wa TRA walioagizwa kuchunguzwa.
“Tupo
kwenye uchunguzi mzito ambao unakusanya mambo mengi sana na hata
inaweza kuongezeka idadi ya watu. Sasa ninachoweza kusema Watanzania
watupe muda kila kitu kinakwenda sawa na tutatoa taarifa ya uchunguzi
wetu,” alisema Advera.
Bakhresa kuchukua hatua
Kwa
upande wake Kampuni ya Said Salim Bakhresa & Co. Limited kupitia
Idara ya Ushirikiano, ilieleza kuwapo kwa ushirikiano baina yake na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika uchunguzi unaoendelea.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa kampuni hiyo itachukua hatua dhidi ya wahusika.
“Wale wote wanaohusika na upotevu huo watachukuliwa hatua na kodi yote
ya Serikali inalipwa na wamiliki wote wa makontena yaliyo husika katika
upotevu huo,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata
hivyo kampuni hiyo ilishangazwa na taarifa za kujumuishwa katika
upotevu wa makontena 349 yaliyoripotiwa hivi karibuni kuwa yametolewa
bandarini bila kulipiwa ushuru.
Novemba
27, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, muda mfupi baada ya
ziara ya kushitukiza ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa aliyofanya
Bandari ya Dar es Salaam.
Taarifa
ya Ikulu iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
imeeleza kuwa hatua hiyo ya Dk. Magufuli imechukuliwa baada ya kubaini
kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipa kodi na
kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 80.
Baada
ya kusimamishwa kazi kwa Bade, Rais Magufuli alitangaza kumteua Katibu
Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango, kukaimu nafasi hiyo hadi
hapo uchunguzi utakapokamilika.
Pamoja
na hali hiyo pia Rais Magufuli, aliiagiza maofisa wote wa TRA
kutosafari nje ya nchi, hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.
Majaliwa
alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa
TRA, kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh
bilioni 80.
Majaliwa
alichukua uamuzi huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya
Bandari (TPA) pamoja na wa TRA, ambapo pia alimtaka Bade na Naibu
Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na polisi
kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na
kurudishwa serikalini.
Kutiwa
jela, kukaguliwa akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi
ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, waziri mkuu aliwataja maofisa
waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu
wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.
“Hawa
wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia
Polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama
zinaendana na kipato cha utumishi wa umma,” alisema Majaliwa.
Maofisa
wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari
(hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD
In-Charge), Eliachi Mrema.
Pia
aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es
Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa
Mwandengele na Robert Nyoni ambao baadaye walitangazwa kusimamishwa kazi
ili kupisha uchunguzi dhidi yao
MTANZANIA

0 comments:
Post a Comment