Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilitishia kumkamata Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred
Lwakatare baada ya kutokuwapo mahakamani hapo.
Kauli
ya Hakimu Thomas Simba imetolewa baada ya Mdhamini wa mshtakiwa,
Paschal Mwita kudai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo hakuwapo
mahakamani na kwamba amesafiri kwenye shughuli zake za ubunge.
Wakili
Mwandamizi wa serikali, Pamela Shinyambala alidai kuwa barua ya ruhusa
ya mshtakiwa huyo ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Bukoba Mjini, ameiona
leo (jana) na kwamba upelelezi haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo
kupanga tarehe nyingine.
Hata
hivyo, Hakimu Simba alionya kuwa ubunge wake (Lwakatare) usiwe sababu
ya kuahirisha kesi hiyo na alipanga kuisikiliza tena Desemba 21 mwaka
huu.
Katika
kesi hiyo, Lwakatare na Joseph Ludovick wanadaiwa kuwa Desemba 28, 2013
katika eneo la King’ongo, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walikula
njama za kujaribu kumdhuru aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
Mwananchi, Dennis Msacky kwa njia ya sumu.
0 comments:
Post a Comment