Tuesday, December 1, 2015

Mwaikimba


Gaudence Mwaikimba ni mwanasoka wa Tanzania kwasasa anacheza kwenye timu ya JKT Ruvu inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, Mwaikimba ni miongoni mwa wachezaji wachache walioweza kudumu kwenye soka kwa muda mrefu. Ameshafikisha miaka 10 tangu aanze kucheza ligi kuu Tanzania bara.


Mshambuliaji huyu mwenye umbo kubwa alijipatia umaarufu akiwa katika klabu ya Yanga ambako alidumu kwa misimu minne (2006-2009), aliichezea pia timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ enzi za kocha Marcio Maximo lakini Mwaikimba ameingia kwenye historia ya vitabu vya Azam FC kwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioipa timu hiyo ubingwa wa ligi ya Vodacom Tanzania bara kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo.

Mtandao huu umemtauta Mwaikimba na kupiganae story ili kujua maisha yake ya soka yalianzia wapi na amepita kwenye vilabu gani kabla ya kutua JKT Ruvu, mafanikio yake ya soka na mambo mengine mengi ambayo ulikua huyafahamu kuhusu maisha ya mwanandinga huyu.

 Shaffihdauda.co.tz: Soka lako ulianzia wapi, umepita kwenye vilabu gani hadi sasa umefika hapa

Mwaikimba: Nimeanza kucheza mpira kuanzia shule ya msingi na sekondari lakini kwasababu ya masomo ya sekondari, kidogo nilisimama ili kupisha masomo yachukue nafasi kubwa lakini baada ya hapo nikaendelea tena na soka.

Nilipomaliza eleimu ya sekondari niliendelea kucheza mpira kwenye timu yangu ya mtaani lakini timu ambayo nilicheza nikaanza kuonekana na wengi ilikuwa inaitwa New Fighters japo kuna timu nyingine nimeshawahi kucheza huko nyuma ambazo siwezi kuzitaja kwasababu ukiwa mtaani unacheza timu nyingi tu.

Mwaikimba 2

Nimecheza New Fighters ikiwa inashiriki ligi taraja la tatu baada ya hapo nikajiunga na Tukuyu Stars, mimi kwetu ni Kyela lakini Tukuyu Stars ni ya Mbeya mjini kwahiyo watu walivyokuwa wananiona nacheza wakaniambia ninauwezo wa kucheza ligi kuu. Baada ya watu kunihamasisha nikaamua kwenda Tukuyu Stars lakini sio kama walikuwa wakinihitaji, nilienda mwenyewe kufanya majaribio bahati nzuri nikakubalika nikaanza kucheza ligi kuu mwaka 2004.

Nilicheza msimu mmoja pale nikaondoka nikaenda Kahama United lakini sikumaliza msimu nikiwa Kahama nikaondoka kwasabau za kimazingira pamopja na akili ya kitoto nikaona kule hakunifai. Baadaye nikajiunga na Ashanti United mwaka 2005 sasa pale akili ilikuwa imekomaa nikawa najua natakiwa nifanye nini baada ya kuondoka Kahama bila sababu za msingi.

Nikiwa Ashanti nikapata akili, nikaanza kuona mpira unaweza kunitoa na kunilipa kwenye maisha yangu, nilicheza Ashanti kwa mafanikio kwasababu timu ndiyo ilikuwa imepanda kushiriki ligi kuu halafu  tulikuwa wachezaji wengi vijana ambao wengine hadi leo bado wanacheza ligi kuu kama mimi,  Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Nyoso, Musa Kipawa na wengine wengi.

Mwaikimba 5

Mwaka 2006 nikajiunga na Yanga na kucheza misimu minne, Yanga nilicheza kwa mafanikio makubwa sana kuna vikombe vya ligi kuu na vikombe vingine tulichukua.

2009 nikaondoka Yanga baada ya ligi kuisha, kocha Julio (Jamhuiri Kihwelo) akanichua na kunipeleka Uarabuni. Akanipeleka Oman nikapata timu lakini bahati mbaya nikaumia goti na kawaida ya waarabu hawawezi kukaa na mtu ambaye ni majeruhi. Walijitahidi kunitibia lakini bahati haikua yangu ikabidi nirudi Bongo. Baada ya kufika  huku nilikuta ligi inaendelea na usajili wa dirisha kubwa ulikuwa umeshapita. Nikaendelea kuuguza goti lakini baadae dirisha dogo nikajiunga na Tanzania Prisons ili kuendelea kuusikilizia mguu wangu.

Nilijiunga na Prisons ili kujaribu kuinusuru isishuke daraja kwasababu ilikuwa kwenye hali mbaya lakini bahati mbaya Prisons ilishuka daraja. Nikatoka Prisons nikaenda Kagera nikacheza msimu mmoja nikacheza kwa mafanikio pia  tukashika nafasi ya nne msimu huo na mimi ilibaki kidogo niwe mfungaji bora lakini nilizidiwa magoli mawili na Ngassa wakati huo alikuwa Azam  alimaliza akiwa na magoli 16 mimi nikafuata kwa magoli 14.

Baada ya hapo tukaenda kucheza mashindano ya Taifa Cup mwaka huo yalifanyikia Arusha nikaisaidia timu yangu ya mkoa wa Mbeya uchukua ubingwa wa Taifa Cup lakini mashindano hayo kwasasa hayapo. Nakumbuka nilikuwa mfungaji bora wa mashindano huku Jerry Tegete akiwa ananifuata kwa karibu, katika mechi sita nilifanikiwa kufunga magoli nane Jerry akanifatia kwa magoli sita.

Baada ya hapo nikajiunga na Moro United nikaanza vizuri pia pale Moro lakini nikaondoka Moro kipindi cha dirisha dogo la usajili nikajiunga na Azam tayari nikiwa nimesha wafungia Moro magoli saba au nane kama sikkosei.  Nikaanza kucheza Azam tangu mwaka 2012 hadi 2015, nimecheza misimu mitatu na nusu, mimi ni miongomi mwa wachezaji walioipa Azam ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya kwanza.

Mwaikimba 1

Nimecheza Azam kwa mafanikio licha ya kuchukua kombe la ligi pia tulifanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya pili mara tatu na kuchukua vikombe vingine kama Mapinduzi Cup mara mbili, tukacheza fainali ya Kagame kwa mara ya kwanza tukafungwa na Yanga.

Baada ya kutoka Azam sasahivi niko JKT Ruvu, hiyo ndiyo historia yangu ya soka kwa kipindi chote tangu nimeanza kucheza soka na kupita kwenye vilabu kadhaa vya Tanzania bara.

Shaffihdauda.co.tz: Wakati unasajiliwa Yanga kutokea Ashanti United ulisajiliwa kwa dau gani kwa wakati huo?

Mwaikimba: Nilisajiliwa kwa dau la shilingi milioni tatu lakini hiyo milioni tatu sikuipata yote kwa pamoja kwasababu kipindi kile Yanga haikuwa na mfadhili kwahiyo viongozi walikuwa wanatoa pesa zao mfukoni na wakati huo Manji alikuwa bado hajaanza kuidhamini Yanya wakati Manji anaanza kuidhamini Yanga mimi tayari nilikuwepo Yanga.

Sisemi kwamba niliondoka Yanga nikiwa nawadai, ila hela yangu niliipata kwa mafungu, lakini nilifurahia kucheza Yanga kwasababu hata mimi nilikuwa na shauku ya kucheza timu kubwa, sikuona sababu ya kukataa na niliona ni watu ambao waliniamini na mimi nikawaamini licha ya kupewa hela yangu kwa mafungu lakini niliipata yote.

Shaffihdauda.co.tz: Kunatofauti gani kati ya Yanga na timu nyingine ambazo umewahi kucheza kama Kagera Sudar, Ashanti, Azam na timu nyingine zote ambazo umewahi kucheza?

Mwaikimba: Utofauti upo kwasababu unapocheza timu kama Yanga au Simba unmakuwa unacheza kwa ajili ya kuufurahisha umati kwasababu hizi timu zina mashabiki wengi sio Dar es Salaam tu bali ni Tanzania nzima kwahiyo kwenye timu hizi kunakuwa na presha kubwa toka kwa mashabiki.

Na presha kubwa inakuwa kwa mchezaji ambaye hajakubalika, unajua ukikubalika Simba na Yanga hata mashabiki wenyewe wanakuwa wanajua mchezaji fulani amekoea kwa bahati mbaya ila fulani hajui na hakustahili kucheza kwenye timu hii.

Mwaikimba 3

Mashabiki wa Simba na Yanga hawakubaliani na matokeo ya kufungwa wenyewe wanataka kushinda kila siku na kila mechi hawajui kama kuna matokeo zaidi ya hayo tena kibaya zaidi mkifungwa na timu ndogo.

Mimi wakati nacheza Yanga nilikuwa na upepo tofautitofauti, leo naweza nikawafurahisha wakanishangilia lakini kuna siku nikawa vibaya nikazomewa na kufikia hatua wanamshinikiza kocha anitoe lakini wakati wananizomea ikitokea nimefunga, haohao tena wanashangilia kwahiyo nikagundua kumbe shida yao ni kuwafungia magoli.

Shaffihdauda.co.tz: Umecheza timu nyingi sana kwenye ligi ya Tanzania bara na kufanikiwa kupita kwenye timu za majeshi, kuna tofauti gani kati ya timu hizi na timu nyingine za wanachama au watu binafsi kama Azam?

Mwaikimba: Kwanza kabisa hizi timu za majeshi kitu cha mbele kabisa ni nidhamu, huwezi kucheza timu za majeshi kama huna nidhamu. Lakini mimi nashukuru nidhamu yangu kwenye soka ipo juu ndio maana nimedumu kwenye soka kwa muda wa zaidi ya miaka 10, na kuwepo kwangu hapa JKT ni sehemu sahihi. Awali walikuwa wanahofu kwamba nimetoka kwenye timu yenye jina kubwa labda ningewasumbua lakini haijawa hivyo.

Tangu nimejiunga na JKT Ruvu sijawahi kulalamikiwa kwa kesi yeyote ya kinidhamu wasababu najua silaha ya mchezaji ni nidhamu na timu za jeshi zipo kwenye mlolongo wa nidhamu, hata timu za kawaida zinasisitiza nidhamu lakini hazifatilii kwa vitendo. Kuna baadhi ya wachezaji kwenye timu nyingine wanaoonekana wanazisaidia sana timu hawaadhibiwi hata wakiwa na nidhamu mbovu.

Unakuta mchezaji haonekani mazoezini, anakunywa pombe hovyo lakini siku ya mechi anapangwa, tofauti na timu za jeshi hata uwe nani kama nidhamu yako mbovu basi utaahibiwa tu.

Shaffihdauda.co.tz: Ni mafanikion gani ambayo unajivunia hadi sasa uliyoyapata kutokana na kucheza mpira?

Mwaikimba: Yapo mengi lakini kikubwa ni kwamba jamii inanitambua hata nikipita sehemu ya watu watano basi wawili au watatu kati yao wanaweza wakawa wananitambua kwamba yule ni Mwaikimba.

Mwaikimba 4

Nimefanikiwa kidogo kwenye maisha, kwasababu kwa mpira wa Tanzania ukiwa na sehemu yako nzuri ya kuishi (nyumba) na sehemu zako ulizoziandaa kukupatia kipato kidogokidogo unapata hela ya chai bila kuomba ni jambo zuri kwasababu nina asset zangu ambazo siwezi kuzisema nina usafiri wangu lakini kikubwa zaidi ni kufahamika na jamii, hata leo nikipata tatizo naweza kusaidiwa kirahisi.


0 comments:

Post a Comment