Posted by Williammalecela.com on Friday, December 11, 2015


 |
VMM/U.80/8/Vol.I/42 11/12/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu zangu waandishi wa habari, Nawapongeza sana kwa namna
mlivyojipambanua katika kuhakikisha mnaitumikia nchi yenu kwa kufanya
kazi kwa utaalamu wa hali ya juu unaotokana na Taaluma zenu.
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi kwa mwendelezo ule ule wa
kuhakikisha inaendelea kutoa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Ilani
ya CCM kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha yale yote
tuliyowaahidi wananchi wakati wa kampeni tunayatekeleza kwa umakini na
kasi kubwa.
Ndugu waandishi wa Habari Umoja wa Vijana wa Chama
cha Mapinduzi tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwa uteuzi mahiri na makini wa Baraza la Mawaziri
aliloliteua tarehe 10/12/2015, ni Baraza dogo lakini lililokamilika
katika kuhakikisha linagusa kila Sekta. Pia ni Baraza linaloakisi adhma
ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha anaendelea kupunguza na kubana
matumizi yasiyo ya lazima.
Tumeridhishwa na uteuzi huu ambao
umesheheni Mawaziri na Manaibu Waziri wenye uwezo na weledi mkubwa sana,
na hatuna mashaka kwamba watafanya kazi kwa kasi na uzalendo. Lakini
pia Umoja wa Vijana tumefarijika zaidi kwa Baraza hili kuwa na Vijana
wengi, kwa hakika tunaiona dhamira ya dhati ya Mh. Rais Dr. John Pombe
Magufuli ya kuhakikisha Tanzania inapata mabadiliko ya haraka, sote
tunaamini Nguvu Kazi ya Taifa letu ni Vijana, na tuwaombe Vijana wote
mliopewa nafasi na Mheshimiwa Rais mtambue kwamba kawaamini sana kwa
hiyo ni mategemeo yetu hamtotuangusha.
Ndugu zangu waandishi wa
Habari, Umoja wa Vijana wa CCM inachukua fursa hii kuwataka Mawaziri
wote walioteuliwa watekeleze Ilani ya CCM kwa kasi ambayo ameanza nayo
Mheshimiwa Rais katika maeneo mbalimbali, Changamoto ni nyingi sana na
Ilani ya CCM imeainisha kinagaubaga ni mambo gani ya msingi Serikali ya
awamu ya Tano inatakiwa kuelekeza nguvu zake zote ili kuhakikisha
inamkwamua Mtanzania kwenye dimbwi la umaskini, lakini sisi kama wadau
wa Vijana tunaomba Mawaziri husika wamsaidie Rais kutatua changamoto za
Vijana ikiwemo changamoto kubwa ya AJIRA. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
imeainisha namna gani Serikali itatatua changamoto hii, Mawaziri husika
wahakikishe wanasimamia kwa nguvu zote katika maeneo yafuatayo:-
-> Kuhakikisha mchakato wa Baraza la Vijana la Taifa unakamilika ili
kuwawezesha Vijana kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli zote za
Baraza la Taifa la Vijana.
-> Utengwaji wa maeneo ya Uzalishaji Mali
-> Kuziwezesha Saccoss za Vijana
-> Kuwapatia mitaji wahitimu wa Elimu ya Juu
-> Kuanzisha vituo maalum vya Vijana kila Wilaya
-> Vijana kunufaika na milioni 50 zitakazotolewa na Serikali kwa kila Kijiji.
-> Vijana kufaidika na shughuli za maendeleo
-> Mafunzo ya TEHAMA na Ujasiamali
-> Vijana kufaidika na Mifuko Hifadhi ya Jamii Vijana kunufaika na Mapato ya kila Halmashauri
->Vijana wajasiliamali kunufaika na manunuzi ya kila Halmashauri
-> Kuondoa kero na malalamiko kuhusu ushuru na kodi zinazotozwa na Halmashauri
-> Mapambano dhidi ya Madawa ya kulevya.
Yote haya na Mengine mengi ambayo Ilani imeainisha ili kuwawezesha
wananchi Kiuchumi Mawaziri husika wanapaswa kutekeleza kwa kasi na nguvu
kubwa ili NGUVU KAZI hii itumike katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.
Ndugu waandishi wa Habari Watanzania tuna kero nyingi sana
zinazotukabili, Serikali itimize wajibu wake wa kuhakikisha inawawezesha
wananchi Kiuchumi lakini Mawaziri wanakazi kubwa ya kuhakikisha
wanaendeleza mapambano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima ili fedha
hizo zielekezwe kwenye kuboresha huduma za Kijamii, Watanzania
hatutawaelewa Mawaziri wetu kama hawatofuata maagizo ya Chama cha
Mapinduzi yaliyoanza kutekelezwa kwa kasi kubwa na Mhe. Rais, na hasa
Vita dhidi ya Rushwa na ubadhilifu wa Mali ya Umma.
Ndugu
waandishi wa Habari Mheshimiwa Rais bado anaendelea na mchakato wa
uteuzi wa Mawaziri katika maeneo ambayo hayajakamilika. Tuna Imani
atakamilisha zoezi hili kwa umakini na umahili kwa vigezo alivyovitumia
kuwapata Mawaziri hawa waliokwishateuliwa, Mungu amuongoze ili Serikali
ikamilike.
Tunawatakia kila la kheri Mawaziri wote katika kulijenga Taifa.
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Egla Obed Mamoto KATIBU IDARA YA UHAMASISHAJI, SERA, UTAFITI NA MAWASILIANO (UVCCM)
|
0 comments:
Post a Comment