Monday, December 28, 2015




Waziri wa wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Ziwa kuhakikisha wanauingiza mkoa wa Kagera katika Gridi ya Taifa baada ya kubainika nchi inaingia gharama kubwa kununua umeme kutoka Uganda.

Alitoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kagera na kusisitiza katika mipango mipya ya Tanesco kwa sasa, ni lazima iondokane na umeme wa gharama kubwa.

Katika ziara hiyo ambayo alikagua mitambo ya kusambaza umeme katika wilaya za Bukoba, Biharamulo na Ngara, Muhongo alisema umeme unaonunuliwa kutoka Uganda wa megawati 5.2 , kila uniti hununuliwa senti nane za Kimarekani.

Aliagiza kwamba kabla ya Tanesco kusaini mkataba mpya na Uganda, wanapaswa kusaini mkataba wa muda wakati wakiendelea kuweka utaratibu wa kuhamishia mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa. Alisema mkoa huo ukiingizwa kwenye gridi, Tanesco itaepuka gharama kubwa za kunununua umeme wa gharama ya juu kutoka nchi hiyo.

Alisema kwa sasa Gridi ya Taifa imefika Nyakanazi, wilayani Biharamulo. “Kwa hiyo hata wilaya nyingine hazina budi kuingizwa katika gridi ili kufanya mkoa uwe na umeme wa uhakika na wa bei nafuu utakaowafanya wananchi kuzalisha kwa kutumia umeme…,” alisema.

0 comments:

Post a Comment