Monday, December 28, 2015

Waganga wa Tiba Asili Nchini wamepinga tamko la Serikali lenye maagizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku waganga hao kujitangaza katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
 
Waganga hao wamefikia uamuzi wa kupinga agizo hilo la serikali kwa madai kwamba agizo hilo halikushirikisha wadau wote na halikuzingatia sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala

Wakizungumza kwenye mkutano ulifanyika jana kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam waganga hao kwa pamoja walisema agizo la serikali linaonesha ni kiasi gani wanadharaulika na serikali haijali mchango wao katika jamii na taifa.

Aidha, waganga hao walisema kwamba uwepo wao hapa nchini unalindwa na sheria zilizopo hivyo uamuzi wowote dhidi yao ulipaswa kutangazwa tofauti na ilivyofanya serikali kwa kuwaagiza kupitia vyombo vya habari.

Miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo na mdau wa tiba asili Boniventure Mwalongo alisema wao kama waganga wa tiba asili na tiba mbadala hawakubaliani na agizo hilo la serikali kwa kuwa hawakushirikishwa

Naye Mkurugenzi wa Ulcers Clinic Tabibu Rahabu Rubago alieleza jinsi alivyosikitishwa na taarifa za agizo la serikali linalowapiga marufuku kujitangaza hali iliyomsababishia kulazwa hospitalini akidai kwamba wakati anasikia taarifa hiyo alikuwa tayari ametoka kulipia matangazo yake ya mwaka mzima katika kituo cha Star Tv.

0 comments:

Post a Comment