Posted by Williammalecela.com on Monday, December 07, 2015
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anatarajiwa kuanza
kambi nzito jijini Arusha kuanzia keshokutwa (Jumatano) kwa nia ya
kuhakikisha kuwa mgombea ubunge wa chama chake katika katika Jimbo la
Arusha Mjini, Godbless Lema anatetea kiti chake kwa ushindi wa kishindo.
Taarifa ambazo tulizipata jana toka kwa
watu wa karibu wa Lowassa zilieleza kuwa (Lowassa) ataungana na timu ya
kampeni ya Chadema kujichimbia jijini Arusha kwa siku zote zilizobaki
za kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo Jumapili ijayo.
Uchaguzi wa kumpata Mbunge wa Arusha
Mjini haukufanyika Oktoba 25, 2015 kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine
nchini kufuatia kifo cha mgombea wa ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.
Kadhalika, ilielezwa kuwa hatua hiyo ya
Lowassa ni muendelezo wa ushiriki wake katika kuiimarisha Chadema kwa
nia ya kuleta ukombozi wa kweli kwa Watanzania.
Hivi karibuni alikuwa Mwanza na Geita
kwa siku kadhaa katika kushughulikia mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chadema mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, ambaye aliuawa kinyama na watu
wasiojulikana.
Katika hatua nyingine, Lema anayegombea
kutetea jimbo hilo,alisema ushindi kwake na chama chake uko wazi kwani
wananchi wameamka na wengi wamepania kumrejesha madarakani.
Alisema kampeni zake za nyumba kwa
nyumba ndizo zinazomuongezea uhakika wa kushinda kwani hupokewa vizuri
na wote humuahidi kujitokeza kwa wingi Jumapili ili kumchagua.
Akizungumza katika mkutano wake wa
kampeni jana, Lema alisema atakapochaguliwa, kazi kubwa atakayoifanya ni
kuhakikisha kuwa mapato ya Halmashauri ya Jiji yanaongezeka ili
kufanikisha dhamira ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment