Dar/Mikoani. Jeshi la Polisi limefanya mabadiliko
kadhaa katika Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwahamisha baadhi ya
askari wake huku wengine wakishushwa vyeo au kuachishwa kazi kutokana na
makosa mbalimbali makubwa yakiwa malalamiko ya kuwaonea wananchi,
rushwa na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara.
Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga akizungumza wiki iliyopita
alisema ili kupunguza rushwa na kuingiza mapato, kikosi hicho
kimeanzisha mfumo mpya wa kulipa faini wa kutumia mashine za EFD, ambao
awali, ulifanywa kwa majaribio na kuonyesha mafanikio licha ya kasoro
kadhaa zilizojitokeza.
Dar es Salaam
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
imeshawabadilisha kazi wakaguzi saba na askari wa vyeo mbalimbali 157 wa
Kikosi cha Usalama Barabarani ambao utendaji kazi wao umeonekana kukosa
tija.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema hivi karibuni
kuwa uamuzi wa kuwabadilisha askari hao kutoka kikosi hicho kwenda
katika kazi za kawaida umetokana na ufuatiliaji wa muda mrefu wa tabia
na mwenendo wao.
Pia, alisema askari ambao watabainika kujihusisha na makosa ya moja kwa
moja ya jinai kama vile rushwa au ukiukwaji wa maadili ya polisi,
watashtakiwa katika mahakama za kijeshi.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu vikosi vingine vya Kanda
Maalumu na Jeshi la Polisi kwa ujumla ili kubaini kama kuna askari,
mkaguzi au ofisa anayefanya kazi chini ya kiwango kisichoridhisha na
ambaye analalamikiwa.
Mtwara
Mkoani Mtwara, jeshi hilo limewabadilisha kazi askari 25 wa usalama
barabarani kuwa askari wa kawaida. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,
Henry Mwaibambe alisema hivi karibuni kwamba sababu kubwa ni kuboresha
utendaji hasa baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kuna
baadhi ya askari wamekuwa wakiomba rushwa na wengine kulipa visasi.
“Tangu tumefanya maboresho haya tuna wiki mbili tu. Baada ya kupata
malalamiko tuliyafanyia kazi ndipo tukagundua kuwa kuna baadhi ya askari
hawafai kufanya shughuli za usalama barabarani tukaona ni bora
tuwaondoe katika kitengo na kuwa askari wa kawaida,” alisema Mwaibambe.
Alisema mabadiliko hayo si wa askari wa usalama barabarani pekee, bali pia yamewakumba wa kitengo cha upelelezi.
Tanga
Mkoani Tanga, polisi imefanya uhamisho wa ndani wa askari wake wa vikosi mbalimbali kikiwamo cha usalama barabarani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Zubery Mwombeji alisema uhamisho huo ulifanyika katika siku za hivi karibuni.
“Ni kweli hatua zimechukuliwa, lakini sheria ya jeshi la polisi
inanikataza kutaja majina ya askari tuliowahamisha kuwashusha vyeo hata
adhabu yoyote, ila nikuhakikishie tu kwamba tumefanya uhamisho mkubwa.”
Kilimanjaro
Askari 38 wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro
wameondolewa kwenye kikosi hicho katika kipindi cha miezi sita iliyopita
na kupangiwa majukumu mengine baada ya kukosa tija na ufanisi.
Morogoro
Mkoani Morogoro, jeshi hilo limewahamishia katika vikosi vingine, askari
60 wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutokana na makosa ya kinidhamu na
kiutendaji.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema si
kila kitu kinachofanyika ndani ya Polisi kinatangazwa kwa jamii.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe alisema
katika kuboresha uwajibikaji kwenye taasisi za Serikali, askari 60 wa
usalama barabarani mkoani hapa waliondolewa na kuhamishiwa vitengo
vingine.
Njombe
Kadhalika, mkoani Njombe jeshi hilo limewabadilisha vitengo maofisa wake
20 wa kikosi cha usalama barabarani kwa lengo la kuongeza tija na
ufanisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Wilbrod Mutafungwa alisema hivi
karibuni kuwa kazi ya kuhamisha askari itakuwa endelevu ili kuhakikisha
wanafanya kazi kwa weledi na maadili yanayotakiwa.
Arusha ngangari
Wakati makamanda wa mikoa kadhaa wakizungumzia kuwahamisha askari hao
kutokana na utendaji usiokuwa na tija, Kamanda Kikosi cha Usalama
Barabarani Mkoa wa Arusha, Harrison Mwakyoma alisema trafiki yeyote
atakayevunja au kukiuka maadili ya kazi atafikishwa mahakama ya kijeshi
kujibu tuhuma zote zitakazomkabili na siyo kuhamishwa.
“Sisi hatuhamishi ila tunaadhibu kijeshi na tunawafikisha kwenye mahakama za kijeshi kwa utovu wa maadili,” alisema Mwakyoma.
Imeandikwa na Bakari Kiango, Mary Sanyiwa, Burhani Yakub, Hamida Shariff, Rachel Chibwete na Zulfa Musa.
0 comments:
Post a Comment