Sunday, December 6, 2015


 
Rais Barack Obama amesema Marekani haitayumbishwa na shambulio la Jumatano katika mji wa San Bernardino, California.

"Sisi tuna nguvu. Tuko imara," amesema kwenye hotuba yake ya kila wiki kupitia redio, akisema inawezekana kwamba watu wawili waliofyatua risasi na kuua watu 14 katika mji huo walikuwa wameingizwa kwenye itikadi kali.

Syed Rizwan Farook, 28, na mkewe Tashfeen Malik, 27, walitekeleza mauaji hayo kabla ya kuuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi kati yao na polisi.

Aidha amefahamika kuwa FBI wanachunguza kisa hicho kama kitendo cha ugaidi.

Kundi la wapiganaji wanaojiita Islamic State Jumamosi lilisifu shambulio hilo na kusema lilitekelezwa na “watu wawili wanaounga mkono Islamic State".

Taarifa hiyo iliyopeperushwa kupitia redio ya IS ya al-Bayan haikutoa ishara zozote kuhusu kuhusika kwa kundi hilo kwenye shambulio hilo katika sherehe ya Krismasi kituo cha Inland Regional Center.

"Tunajua kuwa Islamic State (IS) na makundi mengine ya kigaidi yanawahimiza watu – kote duniani na hata nchini mwetu – kutenda vitendo vibaya vya mauaji, wakati mwingine,” Bw Obama amesema.

"Sote, serikali, idara za usalama, jamii, viongozi wa kidini, tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja kuzuia tusipotoshwe na itikadi hizi za chuki.”


0 comments:

Post a Comment