Licha ya Serikali ya Marekani kuinyima
Tanzania Dola za Marekani milioni 472 (Sh.bilioni999.4) kutokana na kushindwa
kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, lakini imekunwa na kasi ya Rais
John Magufuli katika kupambana vita dhidi ya ubadhilifu na rushwa.
Bodi ya MCC iliyokaa kikao chake
Desemba 16, mwaka huu, iliamua kutopigia kura mkataba unaopendekezwa kati ya
MCC na Tanzania kutokana na kutofurahishwa na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi
Mkuu wa Zanzibar na kukamatwa chini ya kivuli cha Sheria ya Matumizi ya Mtandao
kwa wanaharakati kadhaa Oktoba mwaka huu.
Uchapakazi wa Rais Magufuli kwa kipindi
kifupi alichoingia madarakani tangu Novemba 5, mwaka huu mara baada ya
kuapishwa, umekuwa gumzo kubwa katika baadhi ya nchi barani Afrika na Ulaya
kutokana na kasi yake ya utendaji na kuwaacha viongozi wa nchi hizo kwenye
wakati mgumu.
Mojawapo ya marais ambao wamekuwa
wakilalamikiwa na wananchi wake kutokana na kasi ya Rais Magufuli ni Rais wa
Kenya, Uhuru Kenyata. Kenya ambayo imekuwa ikifuatilia siasa za Tanzania tangu
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, imeonyesha kupenda mbinu za Rais
Magufuli na wananchi wake wanatamani mtu kama yeye.
Nchi nyingine ni Afrika Kusini, Gazeti
la The Sunday Independent linalochapishwa nchini humo, liliwahi kuandika katika
tahariri yake hivi karibuni ikiwa na kichwa cha habari kisemacho, “Afrika
ifuate mfano wa Tanzania.”
Pia sehemu ya tahariri hiyo ilidokeza
kuwa Afrika inahitaji Rais kama Magufuli ambaye ameonyesha kwa dhati nidhamu
katika matumizi ya serikali. Vilevile nchi za Ghana, China nazo zimesifu
uchapakazi wa Rais Dk. Magufuli.
Marekani kupitia Balozi wake nchini,
Mark Childress, imeonyesha kufurahishwa na utendaji wa Rais Magufuli katika
nyanja hiyo ya utumbuaji majipu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Balozi Childress alieleza kuwa Marekani kupitia Shirika lake na MCC
imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli za
kuimarisha vita dhidi ya ubadhilifu na rushwa.
“MCC imetiwa moyo na hatua
zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli za kuimarisha vita dhidi ya
ubadhirifu na rushwa. MCC inatumaini kuwa jitihada hizo zitaendelea na kuleta
mabadiliko ya kimfumo,” alisema.
Balozi huyo alieleza kuwa MCC
inatumaini kuwa jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli kwa sasa zitaendelea na
kuleta mabadiliko ya kimfumo.
Rais Magufuli, Novemba 6, mwaka huu,
siku moja mara baada ya kuapishwa, alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara
ya Fedha (Hazina) kwa kutembea kwa miguu na kutowakuta wafanyakazi wa wizara
hiyo ofisini kitendo kilichomkera.
Mbali na kufanya ziara katika wizara
hiyo, Rais Magufuli Novemba 9, mwaka huu alifanya ziara ya kushtukiza katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako baada ya kushuhudia uozo mwingi
alichukua hatua ya kufuta bodi ya wakurugenzi ya hospitali hiyo na kumuondoa
Kaimu Mkurugenzi wake, Dk. Hussein Kidanto.
Rais Magufuli pia Novemba 7, mwaka huu
alitangaza kufuta safari za nje za watumishi wa serikali hadi pale
atakapotangaza utaratibu mpya.
Alichukua uamuzi wa kufuta safari hizo
kutokana na kuwapo kwa matumizi makubwa ya fedha kwa watumishi wa serikali
walioko katika wizara, taasisi na idara za serikali ambao wamekuwa wakijipangia
safari bila ya utaratibu maalum.
Baada ya kufanya uamuzi huo, Rais
Magufuli alieleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe
na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Siku chache baada ya kutoa agizo hilo,
Rais Magufuli alifyeka msafara wa watumishi wa serikali 50 na kubakia wanne
waliokuwa waende katika mkutano wa Jumuiya ya Madola na kuokoa takribani Sh.
milioni 700 ambazo zinadaiwa zingetumika kwa watumishi hao katika safari hiyo.
Vilevile, Rais Magufuli Novemba 23,
mwaka huu alifuta sherehe za Uhuru na badala yake akaamuru Desemba 9 itakuwa
siku ya kufanya usafi nchi nzima ili kuondokana na tatizo la kipindupindu
linaoikabili nchi.
Uamuzi wake huo uliokoa zaidi ya Sh.
bilioni nne ambazo zilkuwa zitumike katika sherehe hizo na kuelekeza zitumike
kupanua barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam kipande cha kutoka Morocco
kwenda Mwenge.
Mbali na kufuta sherehe hizo, Rais
Magufuli pia alipiga marufuku uchapishaji wa kadi za sikukuu za Krismasi na
Mwaka Mpya kwa gharama ya fedha za umma na kuagiza kila wizara ijigharamie
fedha zake katika kufanya shughuli hizo.
Pia Novemba 20, mwaka huu Rais Magufuli
aliagiza zaidi ya Sh. milioni 200 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya sherehe za
uzinduzi wa Bunge la 11 zitumike kununua vitanda vya wagonjwa katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili.
Rais Dk. John Magufuli Novemba 27,
mwaka huu alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
Rished Bade, baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza
bandarini na kubaini upotevu wa makontena 349 ambayo yalitoroshwa bandarini
hapo bila ya kulipiwa kodi na kusababisha serikali kukosa mapato ya Sh. bilioni
80.
Mbali na kumsimaisha Kamishna huyo,
Desemba 16, mwaka huu, Rais Magufuli alimwondoa aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah kwa kile
alichoeleza kuwa kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza
wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususani kwenye upotevu wa mapato ya
serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment