
Baada
ya kuibua ufisadi wa makontena 2,431 na mengine 349 kupitishwa bila
ushuru, Rais Magufuli alitoa muda wa siku saba kwa wahusika kujitokeza
kulipia kodi, baadhi waliitikia wito lakini inaonekana bado wanajaribu
kujificha.
Jana,
ilibainika kuwa makontena 11,884 na magari 2,019 yenye thamani ya Sh48
bilioni yamepitishwa kwenye bandari kavu bila kulipiwa tozo za bandari.
Ufisadi
huo umeibuka baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
kufanya ukaguzi mwingine katika bandari kavu (ICD) na maghala ya ushuru
wa forodha (CFS) na kubaini upotevu wa kiasi hicho cha fedha.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hatua
zilizochukuliwa na Serikali kuhusu makontena na magari yaliyotolewa
katika bandari kavu na maghala ya ushuru wa forodha ni kuwakamata
watumishi 15 wa Bandari waliohusika katika ukusanyaji wa tozo hizo na
tayari wameshafikishwa polisi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za
kisheria.
“Hii
inatokana na ukaguzi wa awali uliofanyika katika bandari kavu nne
ambazo zilionyesha upotevu wa mapato na ndipo, TPA iliamua kufanya
ukaguzi mwingine katika ICD na CFS zote na hivyo kubaini upotevu wa Sh48
bilioni za mapato ya Bandari,” alisema Profesa Mbarawa.
Makontena
hayo pamoja na magari yalitolewa ICD na CFS baada ya TPA kufanya
ukaguzi katika bandari hizo na kubaini upotevu huo wa mapato.
“Makontena
11, 884 yenye thamani ya Sh47,418,474,795 yalitolewa ICD na CFS bila
kulipia tozo ya bandari na hivyo kuisababishia bandari upotevu wa kiasi
hicho cha mapato,” alisema. “Pia, magari 2,019 yenye thamani ya
Sh1,072,485,518 yametolewa ICD na CFS bila kulipiwa tozo za bandari na
tayari hatua kali tumeshachukua kwa kuwakamata watumishi saba kati ya 15
wa Bandari.”
Profesa
Mbarawa alisema magari yaliyotolewa kutoka kwenye maghala sita ya
ushuru wa forodha bila kulipia tozo ya bandari ni TALL iliyotoa magari
309 yenye thamani ya Sh242,481,207, Chikasa (magari 65, ya Sh16,370,360)
na Farion (magari 18 ya Sh46,390,385).
Magari
mengine ni kutoka ghala la Silver iliyotoa magari 97 yenye thamani ya
Sh168,904,390, Mass (magari 171, ya Sh32,807,115) na Hesu (magari 1,359
ya Sh565,533,061) bila malipo ya tozo za bandari ambazo ni jumla ya
Sh1.07.
Hatua zilizochukuliwa
“Kutokana
na upotevu huo, watumishi 15 wa TPA waliokuwa wanahusika na ukusanyaji
wa mapato hayo, wamekamatwa Desemba 28 (juzi) na kufikishwa polisi ili
wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliwataja
watumishi hao wa Bandari kuwa ni Nathan Edward, John Elisante, Aron
Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Leticia Masaro,
Christina Temu, Merina Chawala, Happygod Naftal, Adnan Ally, Masoud
Seleman, Bonasweet Kimaina, Bernadeta Sangawe na Zainabu Bwijo.
“Serikali
haitamvumilia mfanyakazi yeyote wa TPA awe mkubwa au mdogo ambaye
ataendelea kujihusisha na upotevu wa mapato ya Bandari,” alisema.
Alisema
Serikali itawafutia leseni za biashara mawakala wote wa forodha ambao
wataendelea kushirikiana na wafanyakazi wa Bandari kutoa mizigo bila
kulipia tozo hiyo.
Mawakala na vielelezo
Wakati
huohuo, waziri huyo amewataka mawakala 280 wa forodha ambao
wanatuhumiwa kuhusika na kutolewa kwa makontena na magari bila malipo ya
tozo, kupeleka vielelezo vya uthibitisho ndani ya siku saba kuanzia
jana.
“Watakaoshindwa
baada ya muda huo tulioweka watakamatwa na kufikishwa polisi ili walipe
na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungiwa kufanya
biashara na Bandari,” aliongeza.
Katika
tangazo lake kwenye vyombo vya habari jana, TPA ilitangaza kampuni 243,
nyingi zikiwa za forodha za uchukuzi zikiwamo Ballore Africa Logistics,
Cargo Stars Limited, Mohamed Enterprises Tanzania Limited, Quality
Logistics (T) Limited, Said Salim Bakhresa na Sbc Tanzania Limited,
ikizitaka kupeleka nyaraka zao za kuanzia Julai 2014 hadi Aprili kwenye
ofisi za meneja biashara na masoko kwa ajili ya kuhakiki malipo
waliyofanya TRA.
Naibu
mkurugenzi makampuni ya Said Salim Bakhresa, Hussein Sufiani Ally
alisema makontena yote ya kampuni hiyo yaliyotolewa bandarini
yalilipiwa.
“TPA
wametoa hilo tangazo kwa sababu wanafahamu tumelipa ila wanataka
tupeleke nyaraka zetu kwa sababu wanataka kujiridhisha,” alisema Ally.
Alipoulizwa
kuhusu taarifa ya Profesa Mbarawa aliyotaja Azam ambayo inamilikiwa na
Said Salim Bakhresa kuwa ina makontena 295 ambayo yalitolewa kwenye
bandari kavu bila kulipiwa tozo, alisema hajapata taarifa hizo.
Sh900 milioni zalipwa
Katika
hatua nyingine, jumla ya Sh900 milioni zimelipwa kuanzia Desemba 7 hadi
28, baada ya mawakala wa forodha kulipa tozo ya Bandari kwa makontena
2,431 yaliyokamatwa na Waziri Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza
TPA.
Waziri
Mbarawa alisema kati ya mawakala 55 wa forodha ambao walitakiwa kulipa
kwa hiari ndani ya siku saba, ni saba tu waliolipa kwa wakati kiasi cha
Sh80 milioni.
“Baada
ya muda ulitolewa na Serikali kuisha, mawakala ambao walikuwa
hawajalipa walisitishiwa kufanya biashara na TPA hadi watakapolipa na
tayari hadi juzi askari wamefanikiwa kuwakamata watu 15 kati yao ambao
walilipa Sh820 milioni walizokuwa wanadaiwa na kufanya kiasi
kilicholipwa mpaka sasa kuwa Sh900 milioni,” aliongeza.
Alisema
kazi ya kuwakamata mawakala ambao bado hawajalipa inaendelea na lengo
la Serikali ni hadi kufikia Januari 10, mwakani mawakala wote wa forodha
wawe wamekamatwa na kufikishwa polisi ili walipe kwa nguvu. CHANZO :
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment