SHULE nyingi za msingi na sekondari zisizo za Serikali, zimetuma
maombi kwa Kamishna Mkuu wa Elimu nchini kuomba kibali cha kupandisha
ada katika mwaka ujao wa masomo.
Hatua hiyo ni kuitikia amri ya Serikali ya kuzipiga marufuku shule
binafsi, kupandisha ada kiholela na badala yake shule zote zinatakiwa
kuwasilisha maombi ya kupandisha ada hiyo mpya kwa kamishna huyo ili
yajadiliwe.
“Kwa kweli baada ya tangazo lile shule nyingi zimeleta maombi yao
hapa na kilichobaki ni kwa kamishna wa elimu kuhakikisha anapitia maombi
hayo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyowekwa na Serikali,”
alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Profesa Sifuni Mchome wakati anazungumza na gazeti hili.
Alisema lengo la maombi hayo ni kuondoa tabia ya wamiliki wa shule
zisizo za Serikali, kupandisha ovyo ada kwa kadiri wanavyotaka, jambo
lililosababisha shule nyingine kugeuza elimu kuwa biashara badala ya
kutoa huduma.
Lengo la wizara hiyo ya kutaka maombi hayo na kiwango cha ada
wanazotoza kwa sasa ni kubaini shule, ambazo zinafanya biashara na zile
ambazo zinatoa huduma ya elimu kwa kuisaidia Serikali. Shule ambazo
zitabainika kufanya biashara, zitatakiwa kulipa kodi kutokana na
biashara hiyo wanayoifanya.
Profesa Mchome aliwataka wazazi kuisaidia Serikali kwa shule ambazo
hazitafuata utaratibu huo, watoe taarifa kwa halmashauri za wilaya,
wizarani ili kuhakikisha zile ambazo zimekaidi agizo hilo, zinachukuliwa
hatua.
“Hizi shule ni nyingi ziko zaidi ya 1,000, naomba wazazi watusaidie
kwa shule ambazo zitakaidi agizo la Serikali watuletee taarifa ili
tuweze kuchukua hatua kwa shule husika,” alisema Profesa Mchome ambaye
alisisitiza kuwa wazazi wafanye vikao na shule husika kuhusu
upandishwaji ambao unatangazwa na shule husika.

0 comments:
Post a Comment