Serikali
ya Tanzania imesema imeanza uchunguzi wa ufisadi wa Dola milioni 6
uliohusu mkataba wa mkopo kati ya benki ya Stanbic na serikali hiyo.
Jumatatu,
mahakama nchini Uingereza iliamuru kulipwa kwa fedha hizo kwa serikali
ya Tanzania baada ya taasisi ya uchunguzi wa makosa makubwa ya ufisadi
ya Uingereza kuwasilisha ushahidi kwamba kiasi hicho cha fedha kilipotea
wakati wa uuzwaji wa hati fungani za Serikali kwa benki ya Stanbic
Katibu
Mkuu Kiongozi wa Tanzania Balozi Ombeni Sefue amesema ni uchunguzi wa
benki kuu ya Tanzania katika benki ya Stanbic ndio uliong’amua awali
ubadhirifu huo miaka miwili iliyopita.
Amesema uchunguzi
uling’amua kuwa si tu kwamba Stanbic benki nchini Tanzania iliongeza ada
ya kutafuta mkopo huo kinyemelea lakini pia iligawa nyongeza hiyo kwa
mtu ambaye hakuwa sehemu ya mkataba wa upatikanaji wa mkopo huo.
“Maelezo
tuliyopewa ni kwamba ilibidi kuwepo na wakala wa hapa nyumbani ambaye
ndiye aliyelipwa asilimia hiyo moja iliyoongezwa. Lakini benki ya
Standard ilisema haikumuhitaji huyo wakala, wala sisi hapa
hatukumuhitaji pia. Kwa hivyo ni utaratibu uliofanywa na benki ya
Stanbic hapa Tanzania,” alisema Balozi Sefue
Aliongeza kuwa fedha hizo dola 6 milioni ziliondolewa taslimu siku chache tu baada ya kuwekwa katika akaunti
Mwandishi
wa BBC Sammy Awami anasema hii ni mara ya pili kwa benki hii ya Stanbic
kuhusishwa katika kashfa kubwa ya ubadhirifu wa fedha.
Mwaka jana benki hiyo ilitajwa kutumiwa kupitisha kiasi kikubwa cha pesa kilichohusiana na sakata ya Tegeta Escrow.
Balozi
Sefue ameusifu uamuzi wa makamana na kuyataka mataifa makubwa kuiga
mfano wa namna ya kushughulikia kesi za ufisadi zinazofanywa katika nchi
zinazoendelea.
0 comments:
Post a Comment