KUFUATIA kauli ya aliyekuwa mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mwavuli wa Ukawa, Edward
Lowassa ya kugombea tena urais mwaka 2020, Mkuu wa Oganaizesheni wa
NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura amemhoji Lowassa kama atakuwa tayari
kuendelea kutumikia Ukawa kama jina lake halitapendekezwa kugombea
nafasi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Sungura ambaye alisema anazungumza
siyo kwa niaba ya chama, bali kwa kauli yake mwenyewe, alisema kauli
hiyo ya Lowassa kupambana tena katika kinyang’anyiro cha urais mwaka
2020 kunategemea maamuzi ya chama kupitisha jina lake.
“Nimemsikia Lowassa anasema kuwa anajiandaa kupambana na Rais John
Magufuli mwaka 2020, lakini je, yuko tayari kuheshimu maamuzi ya chama
kwa maslahi ya wakati huo?” Alihoji Sungura.
Sungura alisema mwaka jana jina la Lowassa lilipochujwa kwenye
wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alijiondoa na kuhamia
Chadema.
“Je, atakuwa tayari kuheshimu maamuzi ya chama pale ambapo jina lake
halitapitishwa kugombea urais Chadema au atahamia chama chake?” Alihoji
Sungura.
Akizungumzia ushindi wa viti vya meya uliofanyika mwishoni mwa wiki
iliyopita, Sungura alisema ushindi huo ambao wameshinda wagombea wa
Chadema na CUF usitafsiriwe kuwa ni ushindi wa Ukawa, bali ni ushindi wa
Chadema na CUF .
“Nasema hayo kwa sababu ukizungumzia Ukawa unazungumzia vyama vinne
ambavyo ni Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF, lakini kilichofanyika kuna
baadhi ya kata tulisimamisha wagombea lakini walituwekea kauzibe
tusipate,” alisema Sungura.
Sungura alisema baadhi ya vyama ndani ya Ukawa wana ubinafsi
kuwachanganya watanzania kwa neno Ukawa ambalo halina maana yoyote
badala yake kuviua vyama vingine ndani ya umoja huo.

0 comments:
Post a Comment