MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Rorya, Samwel
Kiboye amesema hatawavumilia watu ambao wamekuwa wakicheza pool muda wa
kazi.
Hayo aliyasema jana kwenye hafla fupi ya sherehe za diwani wa kata ya
Koryo, Peter Sarungi kwa tiketi ya CCM ya kuwashukuru wananchi kwa
kumchagua kuwa diwani wa kata hiyo.
Katika sherehe hizo zilizofanyika nyumbani kwake katika kijiji cha
Koryo, Kiboye alisema uchaguzi umekwisha hivyo hawana budi kuendeleza
shughuli za maendeleo wilayani hapo.
Aliwataka madiwani kusimamia vizuri na kuhakikisha wanachukua hatua kwa watu wanaocheza mchezo huo wakati wa kazi.
“Nimemueleza DC (mkuu wa wilaya) ahakikishe vijiwe vinavyofanywa na
vijana wanashindwa kufanya kazi vivunjwe haraka kwani kukaa vijiweni ni
mwanzo wa uporaji wa vitu ama mali za watu, wamekuwa wakikaa vijiweni
bila kufanya kazi lakini ikifika muda wa chakula wanaenda kuwafanyia
fujo wazazi wao kwa kuwadai chakula,” alisema.
Aliwataka watendaji vijiji na kata kuhakikisha fedha zilizopelekwa
mashuleni zinafanya kazi iliyokusudiwa hususan kuunga juhudi za Rais
John Magufuli.
“Fedha zilizoingia katika shule tumesikia walimu hawajatangazia
wananchi, hivyo naombeni wananchi msimamie kikamilifu, tunamshukuru Rais
kwa uamuzi huu mzuri umesaidia wananchi ambao walishindwa kupeleka
watoto wao shuleni kutokana na michango mingi na hali zao kuwa ngumu,”
alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Milale, Nyawambo Adriano ambaye ni katibu wa
madiwani wa wilaya hiyo aliwaomba wananchi kuwapatia ushirikiano, ikiwa
ni pamoja na kuchangia nguvu kazi katika shughuli za maendeleo badala ya
kuiachia serikali.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Koryo, Peter Sarungi amewapongeza
na kuwashukuru wananchi waliohudhuria kwenye sherehe hizo. Aliwataka
wampe ushirikano ili kuendeleza na kumuunga mkono Rais Magufuli katika
mikakati ya maendeleo ya nchi.
“Kazi ya serikali ni kumalizia kazi na kutoa mwongozo na taratibu za
kazi, hivyo tuondokane na usingizi na dhana za zamani tuliokuwa nao bali
tushirikiane ili tujiletee maendeleo na tuweze kubadili mji wetu wa
Utegi ili usonge mbele,” alisema diwani Sarungi.
0 comments:
Post a Comment