WAFANYAKAZI saba kati ya wanane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
(TPA) waliotuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019
kutoka bandarini ambao walitoroka, wamepatikana na tayari wanaendelea
kuhojiwa na polisi juu ya tuhuma hizo.
Watumishi hao ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa
wameshiriki kuondosha makontena na magari hayo kutoka katika bandari
kavu saba bila kulipa ushuru wa Bandari.
Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi aliliambia gazeti hili jana
kuwa mfanyakazi mmoja kati ya hao wanane, hajapatikana; na anaendelea
kusakwa na polisi ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Wote walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye
huyu alishaacha kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia
suala hilo; lakini bado polisi wanaendelea kumsaka,” alisema Ruzangi.
Mkuu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro
alithibitisha watuhumiwa hao, kukamatwa na kwamba bado wanaendelea
kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.
“Ni kwamba tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Sirro licha ya
kuwa hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao wamepatikana.
“Kwa kweli idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa habari
wiki hii,” alifafanua.
Watumishi waliokuwa wanasakwa na polisi waliopatikana kwa mujibu wa
Ruzangi ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe,
Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward.
Watumishi hao wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante,
Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud
Seleman na Benadeta Sangawe waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo.
Watumishi hao saba, kwa mujibu wa Sirro, tayari walishapelekwa
mahakamani.
“Ukiacha wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao tunaendelea kufanya upelelezi,” alieleza.
Wafanyakazi hao wanatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na
magari 2,019 ambayo yalitoroshwa kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba
bila kulipiwa ushuru wa bandari na hivyo kuipotezea Serikali mapato ya
Sh bilioni 48.55.
Kuhusu mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo
yao makao makuu ya TPA namna ya walivyohusika kulipia makontena hayo,
Ruzangi alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya
suala hilo.
“Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu
mawakala hao, tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja
Mawasiliano huyo.
Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua
ufisadi wa kutisha ambao ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa
kuwashirikisha wafanyakazi wa TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa
Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kwa mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo
kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi. Upotevu huo ulifanya vigogo
wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na makamishna wengine
kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Baadaye Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari.
Katika sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya
biashara na TPA Sakata la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na
magari 2,019, ambayo yaliondolewa kwenye ICD saba bila kulipiwa ushuru
wa bandari na kuipotezea serikali mapato ya Sh bilioni 48.

0 comments:
Post a Comment