Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Mh William Lukuvi amepiga marufuku halmashauri zote nchini kuacha tabia ya kuchukua mashamba ya wananchi masikini bila kuwalipa fidia kisha kupima viwanja na kuviuza kwa bei kubwa huku wanunuzi wa viwanja hivyo majina yakijirudia nchi nzima kwa lengo la kufanya biashara ya ardhi.
Amepiga marufuku hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kibaha
mkoani Pwani saa chache baada ya kuzungumza na uongozi wa mkoa wa Pwani
na serikali ya wilaya ya Kibaha akiagiza mashamba yasiyoendelezwa wala
kulipiwa tozo kwa muda mrefu yakiwemo ya vigogo yatolewe notisi ili
yafutwe na kurudisha mikononi mwa serikali ambapo amesema serikali
haitaki kuwepo na biashara ya viwanja hivyo wizara yake pekee ndiyo
itatoa bei dira ya viwanja.
Awali akizungumza na viongozi wa serikali ya mkoa wa Pwani na
halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mh Lukuvi aliwataka maafisa ardhi
wateule kuhakikisha wananchi waliolipia ada na tozo mbalimbali za ardhi
tangu mwaka 2002 wanapewa hati zao si zaidi ya mwezi mmoja ili
wasifukuzwe kazi na kupunguza chuki na wananchi.
Aidha, Mh, Lukuvi akiwa wilayani Kibaha alitembelea kitovu cha mji
wa Kibaha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko ambao
ujenzi wake licha ya kupata kibali Tamisemi unasuasua ambapo katika
mkutano wake akatoa fursa kwa wananchi kutoa kero na changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika ardhi ili aweze kuifanyia kazi.
0 comments:
Post a Comment