HARUSI
ya karne Bongo ndilo neno linalopendeza kutamkwa kuelezea bonge la
sherehe ya ndoa inayoendelea kuwa gumzo kubwa kwenye vinywa vya wakazi
wengi wa Jiji la Dar es Salaam.
Harusi hiyo ilifanyika Jumamosi
iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar baada ya ndoa kufungwa
kwenye Kanisa la Kristo Mfalme, Tabata kati ya bwana harusi, James
Katagila na bibi harusi, Prugensiana Kahanduka
TETESI ZA AWALI
Mapema
siku hiyo, habari zilitua kwenye dawati la Amani zikieleza kuwa usiku
wa siku hiyo, kutakuwa na harusi ya kukata na shoka kwenye ukumbi huo na
kwamba watu maarufu watahudhuria.
AMANI LATINGA, LASHINDWA KUINGIA
Mapaparazi
wetu walifanikiwa kuwasili kwenye ukumbi huo, saa moja usiku lakini
walishindwa kuzama ndani baada ya ulinzi kuwa wa asilimia mia moja.
NJE YA UKUMBI
Hata
hivyo, nje ya ukumbi huo, magari ya kifahari kama Range Rover, Toyota
Land Cruiser VX na mengineyo mengi yaliegeshwa huku gari la bibi harusi
likiwa ni BMW.
MAHARUSI WAENDA KENYA
Dodosadodosa ya Amani
ilibaini kuwa, licha ya wageni waalikwa kibao kuwemo ndani ya ukumbi,
maharusi walikuwa wakisubiriwa kutoka jijini Nairobi nchini Kenya
walikokwenda kupiga picha kama ‘wanavyoendaga’ ufukweni maharusi wengi
wa Jiji la Dar.
“Humu kuingia jamani ni kazi kama hamna kadi.
Maharusi mnaowaulizia ndiyo wanasubiriwa. Baada ya ndoa, walienda Kenya
kupiga picha,” alisema mwanakamati mmoja aliyekataa kutaja jina lake.
YALIYOJIRI
Kinachofanya
harusi hiyo kuwa ya karne, ni pamoja na mlolongo wake kuonesha tofauti
kubwa na harusi nyingine za Kibongo. Ilielezwa kuwa, mshereheshaji wa
shughuli hiyo, MC Makena alipatikana baada ya watu tisa kufanyiwa
‘intavyuu’, yeye ndiyo akashinda.
MA-DJ 10
Pia, ma DJ
waliokuwa wakitumbuiza kwenye harusi hiyo kwa kuweka CD, walikuwa 10
ambapo kila mmoja alitengewa muda wake wa kupiga muziki na alipomaliza,
hakuwa na kazi tena!
WATUMBUIZAJI
Ili kuifanya sherehe inoge,
wasanii mbalimbali walilipwa fedha kutumbuiza. Wasanii hao ni pamoja na
Josephine kutoka nchini Uganda aliyeimba wimbo wa Kiganda kuhusu harusi
tu.
Mwingine ni JMC kutoka Karagwe, Mkoa wa Kagera. Yeye aliimba nyimbo za Kabila la Wanyambo kutoka mkoani humo.
NYIMBO ZA KIDUNIA
Kwenye
nyimbo za ‘kidunia’, walikuwepo Malaika Band, Kalunde Band na B Band ya
Banana Zorro ambapo wote walitumbuiza kwenye sherehe ya awali kabla ya
maharusi kuingia.
INJILI PIA
Pia kulikuwa na waimba Injili, Rose Muhando na Edson Mwasabwite na waimbaji wao ambao walikonga nyoyo za wahudhuriaji.
KAMERA YA KISASA
Licha
ya kuwepo kwa wapiga picha wa video na picha za mnato, lakini pia ndani
ya ukumbi huo kulikuwa na kamera ya kisasa (drone), inayofanana na
helikopta ndogo ambayo ilikuwa ikipiga picha kutokea juu, ikiongozwa na
mtu aliyekuwa anatumia rimoti.
WATU WALIJISEVIA
Kabla ya
maharusi kuwasili kutoka Kenya, wageni waalikwa walianza kwa kunywa supu
kabla ya kupata msosi na baadaye kukawa na matunda na keki kibao ambapo
watu walielekezwa kwenda kujisevia na kula watakavyo bila kujali muda
maalum.
PETE ZA NDOA
Amani liliambiwa kuwa pete za ndoa za
maharusi zilikuwa na mchanganyiko wa madini ghali ya dhahabu na almasi
hivyo kutoa mwonekano usiozoeleka vidoleni.
SHELA
Ilitonywa
kuwa, bibi harusi alibadili gauni ‘shela’ mara tatu. Alilofunga nalo
ndoa silo alilokwenda nalo kupiga picha Nairobi na silo aliloingia nalo
ukumbini.
Maharusi waliwasili ukumbini hapo majira ya saa mbili usiku
na kupita kwenye zuria jekundu (red carpet) wakiwa wanapigiwa makofi.
SHUGHULI YACHUKUA SAA 12
Mmoja
wa wanakamati wa sherehe hiyo alilihakikishia Amani kuwa shughuli hiyo
iliombewa kibali cha saa 12 ambapo ilianza saa 10 jioni mpaka saa 10
alfajiri siku ya pili ambapo wageni waliondoka baada ya kunywa supu
nzito!
HONEYMOON UGIRIKI
Juzi, Amani lilimtafuta kwa simu
bwana harusi lakini hakupatikana hewani huku habari zikisema yeye na
bibi harusi wapo nchini Ugiriki kwa ajili ya kula fungate (honeymoon) na
wakirudi kuna sherehe kubwa ya kuvunja kamati huku Bendi ya Yamoto
ikitarajiwa kutumbuiza.

0 comments:
Post a Comment