WAZIRI wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, George
Simbachawene amefanya ziara ya kushutukiza katika shule ya msingi Dodoma
Makulu katika manispaa ya Dodoma baada ya kubaini mkuu wa shule
ameitisha wazazi kwa kutaka wachangie.
Suala hilo limekuwa kizungumkuti kufuatia Ofisa Elimu shule ya Msingi
wa manispaa ya Dodoma, Scola Kapinga kuandika barua kwa shule za msingi
katika manispaa yake mkoani hapa kuzitaka kuchangisha michango
mbalimbali.
Hali hiyo kumepelekea Simbachawene akiambatana na Naibu katibu mkuu
Tamisemi Elimu, Bernard Makali kufanya ziara ya kushtukiza katika shule
hiyo ilo kujionea hali halisi ya mgawanyo wa fedha za elimu bure huku
wazazi wakichangishwa .
Waziri huyo akizungumza na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Janeth Justine
alimuhoji kuhusiana na uendeshaji wa elimu katika shule hiyo pamoja na
kutaka kujua idadi ya wanafunzi.
Mwalimu huyo alijibu kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,400 na
ilipokea fedha za elimu bure jumla ya Sh. 152,000 milioni na
walizigawanya fedha hizo kulingana na waraka namba 6 wa serikali.
“Asilimia 30 vifaa, asilimia 30 ukarabati, mitihani asilimia 20
ambapo kwenye michezo ni asilimia 10 huku utawala ni asilimia 10 lakini
pia nilipokea barua toka Manispaa ikielekeza kuwachangisha wazazi fedha
za mlinzi, umeme na maji.
“Nilivyopokea barua niliitisha kikao jana cha wazazi (juzi) ambapo
wazungumzaji alikuwa diwani wa Kata hiyo, Paschal Matula aliwataka
wazazi kukubaliana kutoa michango hiyo mlinzi Sh. 50,000, Maji Sh.
72,000 na umeme kiasi cha Sh 150,000 kwa mwaka,” amesema Mwalimu Janeth.
Hata hivyo amesema kuwa katika kikao hicho hawakufikia muafaka baada ya wazazi kuweka mgomo juu ya kuchangia michango hiyo.
Kufuatia kuwepo kwa michango hiyo Waziri huyo alitoa agizo kwa
Wakurugenzi, wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa nchini kusoma vizuri
waraka namba 6 uliotolewa na Serikali kuhusu mchanganuo wa elimu bure na
kuacha kuchangisha michango wazazi isiyokuwa ya lazima.
“Inaonekana kuna watu wanataka kujinufaisha na michango hiyo kupitia
wazazi kwani michango ambayo wazazi walikuwa wanatakiwa kuchanga tayari
serikali ilishalipa michango yote na walimu wakuu walishakabidhiwa,”
amesema Simbachawene.

0 comments:
Post a Comment