KAZI inayoendelea ya kubomoa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya
yasiyoruhusiwa kisheria, yakiwemo ya mabondeni nchini kote, yataigharimu
Serikali kutumia zaidi ya Sh bilioni moja, MTANZANIA imebaini.
Tayari Serikali imetumia Sh milioni 108.3 hadi jana katika jiji la
Dar es Salaam kwa kipindi cha siku kumi, tangu kazi ya bomoabomoa
ilipoanza katika maeneo ya mabondeni.
Baadhi ya maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na wale wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC),
waliliambia gazeti hili kuwa, hadi kumalizika kwa kazi hiyo Serikali
itakuwa imetumia zaidi ya Sh bilioni moja nchi nzima.
Serikali hutumia Sh milioni mbili kwa siku, kwa ajili ya kulipia magari maalumu ya ubomoaji maarufu kama Tingatinga.
“Fedha nyingine zimeelekezwa kwa wafanyakazi wanaoweka alama ya X
ambao wamekuwa wakibadilika kulingana na kazi inavyokuwa kubwa, ambapo
idadi yao huanzia 50 hadi 80 na hulipwa Sh 50,000 kwa siku,” kilisema
chanzo chetu cha habari.
MTANZANIA ilipotaka kupata ukweli kuhusu gharama za malipo ya wafanyakazi wanaoweka alama ya X
kwenye majengo yaliyojengwa katika maeneo hatarishi ya Gongo la Mboto
na Pugu, mmoja wa maofisa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri
Serikali kulipa kiasi hicho cha fedha.
Wafanyakazi wengine wanaolipwa kwenye kazi hiyo ni askari polisi
ambao idadi yao inakuwa kati ya 30 na 90 kulingana na maeneo yenye
vurugu na yasiyokuwa na vurugu.
Mtanzania limeshuhudia wafanyakazi hao wakilipwa posho zao na
mwakilishi wa NEMC, katika vituo vya Polisi vya Stakishari na Ukonga
jijini Dar es Salaam, baada ya kumaliza kazi.
Taarifa hizo zilieleza kuwa, magari hayo ambayo yamefanyakazi kwa
siku saba yametumia zaidi ya Sh milioni 54, huku mengine yakiwa
hayajafanyakazi ya kubomoa nyumba.
Hata hivyo baadhi ya maofisa hao walishangaa kuona kiwango kikubwa
cha fedha kikitumika kwa kazi hiyo. “Fedha hizi ni nyingi zingeweza
kutengwa kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu na kuhamisha kaya
zaidi ya 8,000,” alisema mfanyakazi huyo.
MCHANGANUO
Mchanganuo wa gharama zilizotumiwa katika siku ya kwanza Serikali
ilitumia Sh milioni 4.5 kwa ajili ya kuwalipa askari 90 ambao kila mmoja
alilipwa Sh 50, 000.
Wafanyakazi wengine 82 walilipwa Sh milioni 4.1 kwa siku hiyo hiyo,
huku magari ya Tingatinga manne yakigharimu Sh milioni nane na kufikia
jumla ya Sh milioni 16.6.
Siku ya pili gharama zilizotumiwa askari walikuwa 60 waliolipwa Sh
milioni tatu, wafanyakazi 74 walilipwa Sh milioni 3.7 na gharama za
magari manne ilikuwa Sh milioni nane, ambazo jumla yake ilikuwa ni Sh
milioni 14.7.
Gharama hizo zilikuwa zikipanda na kushuka kulingana na idadi ya wafanyakazi na gharama nyingine za uendeshaji.
Ukijumlisha gharama zote zilizotumika katika kazi hiyo ya bomoabomoa
na uwekaji wa alama ya X kwa siku 10 iligharimu Sh milioni 108.3 kwa
jijini la Dar es Salaam pekee.
Alama X yaendelea
Akizungumza baada ya kumaliza uwekaji wa alama katika Manispaa ya
Ilala, Ofisa Mipango Miji wa manispaa hiyo, Alfred Mbyopyo, alisema Mto
Msimbazi umeharibiwa vibaya kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga na
kilimo unaosababisha mmomonyoko wa udongo katika kingo za mto.
Hadi jana nyumba ambazo zilikuwa zimewekewa alama ya X kwa maeneo
mbalimbali jijini zilikuwa 16,000 na zile zilizobomolewa zimefikia 700.
KAULI YA SERIKALI
Akizungumzia fedha zinazotumiwa kwenye bomoabomoa inayoendelea, Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula,
alisema anachojua ni kwamba fedha za bajeti huwa hazitumiwi zote
nyingine hubaki kwa kazi za dharura.
Alisema ni ngumu kuelezea moja kwa moja fedha hizo zimetolewa katika
mfuko gani kwa sababu kazi yenyewe inashirikisha wizara zaidi ya nne.
“Kazi hii tunashirikiana na wizara nne ambazo ni Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara Maji na Umwagiliaji”
alisema Mabula.
CHANZO MTANZANIA

0 comments:
Post a Comment