Wednesday, January 27, 2016




SERIKALI imesema itawavua nyadhifa zao Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kushindwa kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari juu ya hali ya ugonjwa wa kipindupindu nchini.

Alisema kuna haja ya kuwachukulia hatua viongozi hao kutokana na kutumia fedha nyingi kutibu ugonjwa huo, lakini matokeo yake wameshindwa kudhibiti. Waziri huyo alisema haiwezekani halmashauri moja inatumia zaidi ya Sh milioni 400 na ugonjwa bado unaongezeka.

“Hawa waganga wakuu kuna haja ya kuwawajibisha, hatuwezi kuvumilia jambo hilo,” alisema Mwalimu. Alisema mpaka sasa zaidi ya Sh bilioni moja zimetumika kwa tiba ya ugonjwa wa kipindupindu ambapo kati ya fedha hizo, Sh milioni 900 zimetolewa na Hazina. “Nitazungumza na Tamisemi kuangalia ni jinsi gani ya kuwachukulia hatua kwani haikubaliki watu waendelee kupokea mishahara kwa kushindwa kusimamia majukumu yao,” alisema.

Mwalimu alisema fedha zilizotumika ni nyingi na kwamba zingeweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo kama wangedhibiti tatizo hilo kwa wakati.

Aliagiza Machi mwaka huu, ugonjwa huo uwe umemalizika na siyo serikali iendelee kupata hasara wakati kuna mikoa imeweza kudhibiti kipindupindu.

Alizitaja mamlaka za mikoa na halmashauri pamoja na watendaji wake kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko wa ugonjwa huo.

Aidha, Mwalimu alisema hadi sasa wagonjwa waliougua kipindupindu wamefikia 14,608 na kati ya hao 228 wamepoteza maisha na kwamba mkoa wa Morogoro unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi. Mikoa mingine yenye ugonjwa huo ni Mwanza, Simiyu, Manyara, Mara, Geita na Mbeya.

0 comments:

Post a Comment