MBUNGE wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) anatarajia kupeleka hoja
binafsi bungeni kuhusu kuanzishwa kwa bandari kavu mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Lusinde alisema uwepo
wa bandari hiyo, utasaidia mkoa huo kukua kiuchumi na wakazi wengi
kupata ajira mbalimbali ili waweze kuondokana na umasikini.
Mbali na kukua kiuchumi, pia ni rahisi kwa nchi jirani na kila mkoa
kuchukulia mizigo yake Dodoma kwa sababu mkoa huo upo katikati ya nchi.
Alisema mkoa huo unatakiwa kupewa hadhi yake kama makao makuu ya nchi
ili uweze kukua kiuchumi, badala ya kuwekeza kila kitu Dar es Salaam
kwa sababu bandari itaweza kuajiri waliosoma na wasiosoma na kufanya
watu kukabiliana na umasikini.
“Nchi kama Rwanda, Burundi, Kongo wataweza kuchukua mizigo yao kwa
urahisi, na hii itatanua shughuli za uwekezaji Dodoma na kuufanya kuwa
mkoa wenye neema. Tumejenga chuo kikuu Dodoma, watu wote hawaingii chuo
kwa kucheza ngoma, wanaingia kwa kusoma, sasa watasomaje wakati hawana
uwezo,” alifafanua Lusinde.
Alisema wakazi wa Dodoma sio wavivu, bali ukame unawafanya kuwa na
maisha magumu, lakini zikitokea fursa za uwekezaji kama huo, wataweza
kuondokana na umasikini.
Lusinde akizungumzia suala la njaa mkoani humo, alisema mkoa huo
unapata mvua kidogo, hali inayofanya kila mwaka kukumbwa na njaa.
Aliiomba serikali ifanye jitihada za kusaidia kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na ukame uliopo.
Alisema inawezekana mkoa huo ukawa wa viwanda na kimbilio kwa
wananchi wa mikoa mingine, endapo hoja yake ya bandari kavu itafanikiwa.
Lusinde aliwaomba wabunge, bila kujali itikadi zao, kumuunga mkono atakapowasilisha hoja hiyo kwa maslahi ya taifa.

0 comments:
Post a Comment