KUHAMA kwa mawaziri wakuu wastaafu kutoka chama kimoja cha siasa
kwenda kingine kumezua mjadala bungeni baada ya Mbunge wa Dimani, Hafidh
Ali Tahir (CCM) kutaka Serikali ifanye marekebisho ya sheria ya mafao,
stahiki zao zifutwe.
Hoja hiyo ilisababisha wabunge wa upinzani akiwemo Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR
Mageuzi) kumjibu Tahir kwa nyakati tofauti kupitia maswali ya nyongeza
wakimshutumu kuwa ni mchochezi na hajui Katiba.
Akijibu swali la Tahir, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki alisema kujiunga na
chama chochote au kujihusisha na masuala ya kisiasa ni haki ya kikatiba
ambazo haziwezi kuzuiwa au kuingiliwa.
Katika swali lake, Tahir alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya
wanasiasa hususani mawaziri wakuu wastaafu ambao wameaminiwa na
kuchaguliwa na wanachama wa chama fulani, lakini baada ya kupata
madaraka huhama vyama na kwenda kunufaisha vingine.
“Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati sasa wa kufanyia marekebisho
sheria husika ili kufuta stahiki za mawaziri wakuu wastaafu wanaohama
vyama vyao kwa kuwa stahiki hizo zilitokana na nguvu za chama
alichohama. “Na kwamba kuendelea kumpa stahiki hizo ni sawa na
kuwakejeli na kuwadharau wananchi waliomchagua?” Alihoji Tahir.
Waziri alifafanua kuwa mawaziri wastaafu wanahudumiwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mafao kwa hitimisho la kazi viongozi, Namba 3 ya mwaka 1999.
Alisema sheria haielezi hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa Waziri Mkuu
mstaafu atakayeamua kuhamia chama kingine cha siasa tofauti na chama
kilichomweka madarakani na kumwezesha kushika wadhifa wa Waziri Mkuu.
“Mbali na sheria hiyo kutoweka zuio lolote kwa viongozi wa kitaifa
wastaafu kujiunga na chama kingine cha siasa, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inalinda haki za msingi za binadamu
ikiwemo haki ya uhuru wa mtu kujihusisha na masuala ya kisiasa,”
alisema.
Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai alimshukuru Naibu Waziri kwa majibu
aliyotoa huku akisema tatizo si la mbunge aliyeuliza pekee bali ni la
nchi nzima. Kuhusu shutuma kwa watumishi wa umma kwamba hawatendei haki
vyama vingine, waziri alisema watumishi wanatambua vipo vyama vingi na
ipo ilani ya CCM ambacho ndicho chama tawala. Alisisitiza wanachotakiwa
kufanya ni kutekeleza sera za serikali.

0 comments:
Post a Comment