Wednesday, January 27, 2016




KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amehoji ni kwa nini serikali isiweke mpango maalumu kupitia halmashauri za wilaya wa kuangalia namna ya kuhifadhi maji ya mvua ili yasilete maafa na yatumike katika kilimo.

Akiuliza swali la nyongeza jana bungeni, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai (Chadema), alisema ni vyema serikali ikaanzisha mpango huo ili kuhifadhi maji wakati wa mafuriko ambayo pia yatasaidia kuondokana na tatizo la chakula.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema serikali italeta wazo la kuvuna maji ya mvua katika awamu ya pili ya mpango wa maji unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Lwenge alizitaka halmashauri zote nchini kila mwaka kuwa na mpango wa kujenga mabwawa madogo madogo ili kuhakikisha madhara yatokanayo na mvua yanaepukwa. Pia alisema serikali itaendelea kusimamia miradi mikubwa ya maji iliyoko nchi nzima na kuhakikisha inakamilika.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha wananchi wanapata maji kwa asilimia 100. Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) aliyetaka kufahamu lini serikali itatekeleza Sera ya Taifa ya Upatikanaji Maji nchini ya Mwaka 2002.

Lwenge alisema Sera ya Maji ya Mwaka 2002 inatamka wazi kuwa umbali wa upatikanaji wa maji uwe mita 400 jambo ambalo serikali imeshaanza kutekeleza tangu mwaka 2007 katika awamu ya kwanza ya mpango huo ingawa hawajafikia lengo, hivyo wataendeleza katika awamu ya pili ya mpango inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Azza Hamad (CCM) aliyetaka kufahamu serikali itakamilisha lini mradi wa maji wa kisima kirefu katika Mji Mdogo wa Tinde.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema serikali imepeleka Sh milioni 200 ambazo zimepokewa Novemba 2015 zitakazotumika kununua na kufunga pampu na mfumo wa umeme wa jua pamoja na miundombinu yote na kazi hiyo inayofanywa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHIUWASA) itakamilika Aprili 2016.

0 comments:

Post a Comment