MTANDAO wa Wasanii Tanzania (Shiwata) umeamua kumpa uanachama wa
heshima mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani, Mbwana
Samatta pamoja na kumzawadia ekari tano za ardhi katika kijiji cha
Wasanii Mwanzega, Mkuranga kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya
soka.
Mwenyekiti wa Shiwata, Cassim Taalib alisema jana kuwa kikao cha
Kamati Utendaji ya Mtandao huo kilichoketi juzi kilifikia uamuzi huo
baada ya kufuatilia kwa karibu mafanikio ya Samatta akiwa na timu ya
Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kufanya vizuri katika mashindano ya
Afrika hadi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora.
Alisema Shiwata inatoa kiwanja hicho kama zawadi kwa mchezaji huyo
kutokana na uwezo wake wa kulitangaza taifa katika medani ya kimataifa
katika mchezo wa soka ambako wengine watafuata nyayo zake.
Taalib alisema taratibu za makabidhiano zinafanywa kwa mawasiliano na
baba yake mzazi, Ali Samatta na atakabidhiwa eneo hilo mara baada ya
kurudi kutoka Ubelgiji ambako anaenda kusaini mkataba na timu ya KRC
Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Shiwata yenye wanachama zaidi ya 8,000 inamiliki ekari 300 za kujenga
makazi, kumbi za starehe, viwanja vya michezo na nyumba za kuishi
katika kijiji cha Mwanzega wilayani Mkuranga na ekari 500 eneo la
Ngarambe kwa ajili ya kilimo.

0 comments:
Post a Comment