MAMLAKA ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kushuka kwa bei
za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei nchini.
Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix
Ngamlagosi alisema, licha ya kushuka kwa bei hizo za mafuta katika soko
la dunia, hazitakuwa zikishuka kwa wakati huo huo nchini.
“Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha
bei hapa nchini japo si kwa wakati huo,” Ngamlagosi alisema.
Ngamlagosi alisema kumekuwa na upotoshaji kwamba Ewura haishushi bei
za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaathiri mapato yake, lakini ukweli
ni kwamba tozo ya Mamlaka hii inatokana na lita za mafuta na si bei.
“Iwapo Ewura ingetaka mapato mengi, basi ingeongeza wingi wa lita za
mafuta yanayoingia hapa nchini, na si kutegemea kupanda kwa bei. Hivyo
basi kushuka au kupanda kwa bei hakuna uhusiano wowote na ongezeko la
tozo kwa Ewura,” alieleza.
Alisema, Mamlaka hiyo itaendelea kutimiza wajibu wake kisheria katika
sekta ndogo ya mafuta hapa nchini, ikiwemo upangaji bei kikomo za
mafuta na kuzisimamia katika maeneo yote nchini.
Mkurugenzi huyo alisema kwa mwaka huu, bei ya petroli ilishuka toka
kiwango cha juu zaidi, Septemba 2014, Sh 2,267 kufikia Sh 1,898 kwa lita
ikiwa ni kupunguka kwa Sh 369 kwa lita. Bei ya dizeli ilishuka toka
kiwango cha juu zaidi, Aprili 2014, ilipokuwa ikiuzwa Sh 2,149 na
kufikia Sh 1,747 kwa lita Januari 2016, hii ikiwa ni kupungua kwa Sh 402
kwa lita.

0 comments:
Post a Comment