Thursday, January 28, 2016




WABUNGE wamesema kasi ya utendaji ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, inatoa mwanga wa kuiwezesha nchi kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa (2020-2025) baada ya miaka kumi.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamesema pamoja na mafanikio yanayoanza kuonekana, hasa matumizi ya vitendo ya kauli ya “Hapa Kazi Tu”, kumekuwa na baadhi ya dosari, wakidai serikali haizingatii sheria, kanuni na utaratibu katika baadhi ya uamuzi.

Waliyasema hayo wakichangia katika mjadala wa Bunge wa juzi jioni, mjini Dodoma. Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda alisema matumaini ya sasa ya watanzania ni makubwa na baada ya miaka 10 nchi itakuwa imepiga hatua kubwa na kuufikia dira ya maendeleo ya mwaka 2020-2025.
Alisema hilo linawezekana kutokana na Rais Magufuli kuanza kuboresha huduma za kijamii na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, jambo ambalo linaashiria matokeo makubwa katika kupunguza umaskini.

Mbunge Anna Lupembe (Viti Maalumu -CCM), alisema Rais Magufuli amefanya kazi kubwa hasa kwa kutumbua majipu makubwa ya watu ambao walikuwa hawalipi kodi na matokeo yameonekana.
Pia alitaka ifike wakati maeneo ya wakulima na wafugaji yaainishwe ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara sambamba na kuimarishwa kwa njia ya reli.

 Naye Mbunge wa Mpanda Mjini, Selemani Kapufi (CCM) amewataka wabunge kutokuwa walalamikaji juu ya changamoto za sera ya elimu bure inayotekelezwa na serikali, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa ni sehemu ya tatizo.

Pia alitaka serikali kuunganisha kwa lami mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora ili wakulima waweze kuuza mazao yao kwa wakati. Mbunge wa Babati Mjini, Cecilia Parreso (Chadema), alisema Serikali ya Rais Magufuli imekuwa ikiongozwa na kaulimbiu ya hapa kazi tu, lakini haizingatii na kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Alisema Rais anapomfukuza mtumishi wa umma taratibu za kiutumishi zinatakiwa kufuatwa pia alisema anashangazwa fedha za elimu bure zilizotolewa na serikali kutopata idhini ya Bunge. “Mnapeleka fedha kwa bajeti ipi? Alihoji mbunge huyo.

0 comments:

Post a Comment