Thursday, January 28, 2016




BAADA ya wakulima wa mirungi wilayani Same kupuuza agizo la kung’oa zao hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, inajipanga kufanya kampeni ya kushitukiza kufyeka na kuwakamata wakulima wa zao hilo katika vijiji 28 kata 13 zinavyolima zaidi hilo wilayani hapa.

Pamoja na hilo, Polisi mkoa imemkamata na kumfikisha mahakamani Diwani wa Kata ya Pasua Manispaa ya Moshi, Charles Mkalakala kwa tuhuma za kuizuia isikamate watuhumiwa wa uuzaji na usafirishaji wa mirungi.

Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla amesema kamati yake inaandaa kampeni maalumu ndani ya siku tano kuanzia sasa ili kutokomeza kilimo hicho kinachotishia nguvu kazi ya vijana.

Akizungumza katika kikao maalumu cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wilayani Same kuhusu “Operesheni Mirungi Same,” na kushikirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, madiwani, watendaji wa kata na vijiji, Makalla alisema katika mashamba 921 yaliyotakiwa kufyekwa ni mashamba 313 yaliyofyekwa sawa na asilimia 34 tu.

Katika kikao hicho ambacho pia kiliwashirikisha wenyeviti wa vijiji na wakuu wa vituo vya polisi, Makalla alisema serikali haiwezi kuvumilia kuwepo kwa mashamba hayo huku wananchi wakikaidi maagizo halali ya serikali.

“Baada ya siku tano kuanzia leo kamati yangu imejipanga kufanya operesheni kabambe ya kuhakikisha mashamba yote yaliyobaki yanafyekwa na wananchi watakaokaidi kutekekeza katika siku tano watakamatwa na kufunguliwa mashitaka na kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya adhabu yake ni kifungo cha miaka hadi miaka 30 jela,” alieleza mkuu wa mkoa.

Aidha, mkuu wa mkoa ameagiza watendaji, madiwani na wakuu wa vituo vya polisi kuhamasisha wananchi kutumia siku tano kufyeka na kung’oa mirungi yote kabla sheria haijafuata mkondo wake.

0 comments:

Post a Comment