UCHAGUZI wa mameya katika Manispaa za Ilala na Kinondoni jijini Dar
es Salaam ni wa vuta nikuvute na sasa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene
ameingilia kati.
Waziri huyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik
kuhakikisha kabla ya Januari 16, mwaka huu uchaguzi wa mameya katika
manispaa hizo, uwe umefanyika. Simbachawene alisema hayo jijini Dar es
Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema hadi leo uchaguzi wa mameya katika manispaa hizo, umeshindwa
kufanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa mvutano wa
vyama vya siasa juu ya uhalali wa wajumbe, wanaotakiwa kushiriki katika
kupiga kura; na mapingamizi kadhaa ya kisheria mahakamani.
Aidha alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibari ya mwaka 2010, muundo wa serikali
za mitaa Zanzibar na Tanzania Bara, si jambo la Muungano.
Simbachawene alisema sheria za serikali za mitaa, zimebainisha kuwa
wabunge wa viti maalumu kuwa wajumbe wa baraza la madiwani la
halmashauri za wilaya; na sheria hizo zinaruhusu wabunge wa viti maalumu
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuingia na kuwa wajumbe wa baraza la
madiwani kwenye mamlaka za serikali za mitaa katika ngazi ya wilaya.
“Kwa kuzingatia vifungu hivi vya sheria za serikali za mitaa, wabunge
wa viti maalumu wanakuwa wajumbe wa baraza la madiwani kwa misingi ya
mapendekezo ya vyama husika, lakini lazima mchakato wa kupatikana kwao,
uwe ulianzia kwenye mamlaka hiyo ya serikali za mitaa kwa mfano wilaya,
mji, manispaa au jiji husika,” alisema.
Alisema kutokana na maelezo aliyoyatoa, kwa namna yoyote ile,
haiwezekani kwa mbunge au mbunge wa viti maalumu kupiga kura nje ya
halmashauri ya wilaya aliyokuwepo, wakati anapendekezwa na chama chake
ili kupata nafasi ya uongozi.
“Napenda kuviasa vyama vya siasa kuheshimu sheria zilizopo ili
kujenga, kukuza na kudumisha demokrasia, lakini pia kuondoa na kuepusha
migogoro na mivutano isiyo ya lazima baada ya kumalizika kwa uchaguzi
mkuu wa 2015,” alisema Simbachawene.
Uchaguzi waahirishwa tena Agizo hilo la Waziri, limekuja baada ya
uchaguzi wa mameya, uliotakiwa kufanyika jana, kuahirishwa kutokana na
pingamizi, lililowekwa mahakamani kuhusu kuzuiwa kwa uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment