ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova amestaafu rasmi na kuagwa jana huku akikiri kuwa
hatasahau joto la uchaguzi mkuu 2015 lililosababishwa zaidi na mchuano
wa wafuasi wa wagombea urais John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Akizungumza
wakati wa kuagwa kwake na kisha kukabidhi majukumu kwa kamanda mpya wa
kanda hiyo, Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, Kova alisema uchaguzi
huo uliofanyika Oktoba 25, 2015 ni miongoni mwa vipindi vitatu
asivyotarajia kuvisahau katika maisha yake yote ya kulitumikia jeshi la
polisi.
Alivitaja
vipindi vingine asivyovisahau wakati akilitumikia jeshi la polisi
katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa ni tukio la kuvamiwa kwa kituo
cha polisi Stakishari lililoacha vifo kwa baadhi ya askari wake na pia
ajali ya helikopta.
Akieleza
zaidi kuhusiana na uchaguzi mkuu, Kova alisema uchaguzi huo ulimpa
changamoto kubwa kutokana na wagombea hao kuungwa mkono na watu wengi
kiasi cha kuhofia kutokea machafuko, hasa kutokana na kuwapo kwa mwamko
mkubwa wa kisiasa miongoni mwa wafuasi wa wagombea.
Hata
hivyo, Kova alisema anashukuru kuwa serikali iliwaunga mkono vya
kutosha katika kulinda usalama na hivyo kufanikisha uchaguzi huo kwa
ufanisi.
“Napenda
kuishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia jeshi la polisi
wakati wa uchaguzi kwa kutuongezea vifaa vya kazi kama magari ya
kufanyia doria, silaha pamoja, kwani vilituwezesha kufanikiwa kulinda
amani na utulivu wa hali ya juu,” alisema Kova.
AMTAMBULISHA KAMANDA SIRRO
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova alimtambulisha rasmi jana Naibu Kamishna wa Polisi Sirro, kuwa mrithi wa wadhifa wake.
Akiongea
na waandishi wa habari juu ya hatua hiyo, Kova alisema kwake yeye,
kukabidhi madaraka kwa Kamanda Sirro ni kitendo cha kihistoria kwani
ilikuwa ni ishara ya kuhitimisha salama utumishi wake ndani ya jeshi
hilo.
“Ni
siku ya kihistoria katika maisha yangu kutokana na tendo hili. Lakini
naahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kila namna kwa Kamishna Sirro,”
alisema
ALIKOTOKEA
Akisimulia
safari yake ndani ya jeshi la polisi kwa ufupi, Kamanda Kova alisema
kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Kandaa Maalumu ya Dar es
Salaam, aliwahi kuwa katika idara ya upelelezi kwenye mikoa ya Arusha,
Kigoma, Mwanza, Kinondoni (Magomeni) na baadaye kuwa Kamanda wa Polisi
katika Mkoa wa Mbeya.
“Nina
utumishi wa miaka 40 ndani ya jeshi la polisi na nilikuja kuwa Mkuu wa
Polisi wa Jiji la Dar es salaam (RPC) nikitokea Mbeya mwaka 2008,”
alisema.
MATUKIO STAKISHARI, AJALI HELIKOPTA
Akielezea
matukio ya ajali ya helikopta na uvamizi Stakishari, Kova alisema hayo
hatayasahau kama ilivyokuwa kwa mikikimikiki ya uchaguzi mkuu 2015.
Alisema
tukio la Stakishariu lililowapoteza askari wanne hatalisahahu kwani
hapo kabla alizoea kukabiliana na vitendo vya ujambazi vinavyohusisha
uporaji wa fedha na mali na siyo ugaidi wa kuiba silaha kwenye vituo vya
polisi.
Hata
hivyo, alisema anafarijika kuona kuwa kwa kushirikiana vya kutosha
ndani ya jeshi lao Kanda maaalum ya Dar es Salaam aliyokuwa akiiongoza,
walifanikiwa kuwakamata wahusika wote waliofanya tukio hilo.
Alisema
tukio jingine ni kuanguka kwa helikopta wakati wa kutembelea wananchi
waliokumbwa na mafuriko mwaka 2014 jijini Dar es Salaam, akiwa pamoja na
aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi
ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, John Magufuli na mkuu wa mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadik.
AKABIDHI VYETI
Katika
hatua nyingine, Kova alikabidhi vyeti kwa maofisa 110 wa jeshi la
polisi kutokana na utendaji wao katika hafla ya kumuaga.
Alitumia
fursa hiyo kufanya ukaguzi wa baadhi ya vitu vilivyokamatwa na jeshi la
polisi yakiwamo meno ya tembo, gari mbili, moja likiwa aina ya Toyota
Ford liliibwa nchini Afrika Kusini na Toyota Toyota GX210 ambayo yote
yalikamatwa eneo la Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Kova
alimtaka mrithi wake, Kamanda Sirro kufuata nyayo za uongozi wake kwa
kuendeleza amani na utulivu katika jiji la dare s Salaam kwa kuhakikisha
idadi ya matukio inaendelea kuwa ndogo zaidi.
Kwa
upande wake Kamanda Sirro alimsifu Kamanda Kova kwa kazi yake nzuri
aliyofanya kwa muda wote alipokuwa wakifanya kazi pamoja na kusema kuwa
alikuwa kama mwalimu kwa kila afisa wa jeshi hilo kwa muda mrefu wa
utumishi wake.
Alisema
kuwa amefanya kazi kama kaimu wake wa kanda hiyo kwa miaka miwili, na
kwa muda wote huo kanda hiyo ilikuwa shwari bila kuwepo na wimbi la
machafuko.
“Nimefanya
naye kazi vizuri kwa miaka isiyozidi miwili na amekuwa mwalimu kwangu
na siyo kiongozi tu… ninachoweza kumuahidi ni kuwa nitaendeleza jitihada
za kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment