ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa,
Edward Lowassa, amesema mameya na wabunge wa chama hicho wakishindwa
kuwajibika watafukuzwa uanachama.
Lowassa alisema wabunge na mameya wa Ukawa, hususani wa Chadema
wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wananchi waone tofauti kati yao na
wale wa CCM walioongoza kwa muda mrefu Jiji la Dar es Salaam, lakini
limeshindwa kupiga hatua.
Mwanasiasa huyo pia aligusia ubomoaji wa nyumba za mabondeni na
sehemu zisizoruhusiwa, kwamba licha ya kutekeleza sheria, lakini lazima
ufanywe kwa kuweka mbele ubinadamu.
Akizungumza katika kikao maalumu na mameya pamoja na manaibu wao
kutoka manispaa za Kinondoni na Ilala, Lowassa alisema itakuwa ni aibu
Dar es Salaam kuendelea kuwa chafu na kuzalisha ugonjwa wa kipindupindu.
Lowassa ambaye ni ni Waziri Mkuu mstaafu, alisema Kamati Kuu ya
Chadema ilikwishatoa mwongozo kwa wabunge wake ambao watashindwa
kuonyesha uwezo wa kufanya kazi za wananchi katika mwaka wa kwanza na wa
pili wataondolewa ndani ya chama hicho.
“Hili ni agizo la Kamati Kuu kwamba mbunge na hata meya wakishindwa
ku-perfom, ikipita mwaka mmoja au miwili hawajafanya chochote
watafukuzwa kwenye chama.
“Chadema si chama cha kuendelea kuwa cha upinzani, tunajenga chama
kinachojiandaa kushika dola muda wowote itakapopatikana fursa. Tunataka
kuithibitishia dunia kwamba tunaweza kuongoza dola muda wowote zaidi ya
CCM,” alisema Lowassa.
Pamoja na mambo mengine, Lowassa alitoa maagizo kwa mameya hao wa
Ukawa kukusanya mapato na kuibua miradi mikubwa yenye masilahi kwa
wananchi.
“Mkubaliane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili wakuu wa mikoa na wilaya wasiwazuie
kufanya kazi zenu,” aliwaambia huku pia akiwasisitiza kuweka kipaumbele
kumaliza uchafu na kuimarisha usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
“Mapato hayaonekani, kusanyeni mapato kuliko wakati wowote. Pia
ondoeni sheria ya mhimili yaani wakuu wa mikoa na wilaya, hawa ni wavivu
watawazuia katika spidi ya maendeleo yenu.
“Muondokane na sheria inayowazuia kukopa benki, kopeni benki na chagueni miradi ambayo inawagusa wananchi,” alisema.

0 comments:
Post a Comment