Lakini
naibu waziri huyo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne amesifu hatua
mbalimbali za kupambana na ufisadi anazochukua Rais Magufuli akisema
amefanikiwa kutumbua majibu, lakini sasa anatakiwa awe na ubunifu katika
kutatua matatizo ya wananchi.
Dk
Mahanga alikuwa Naibu Waziri wa Lazi na Ajira tangu mwaka 2008 na
hakuwahi kuhamishwa wala kupandishwa hadi ngazi ya uwaziri hadi Serikali
ya Rais Jakaya Kikwete ilipomaliza muda wake na baadaye kujiunga na
Chadema.
Akizungumza
na Mwananchi jana, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Segerea (CCM)
alisifu kazi inayofanywa na Rais Magufuli akisema inaonekana wazi.
“Kweli ametumbua majipu ambayo hakika yalikuwa yameiva,” alisema Dk Mahanga.
“Naweza
kusema alikuta nyumba chafu na inanuka, ameisafisha. Sasa tunapenda
kuona baada ya kusafisha ataiweka katika hali gani? Atabuni nini ili
kuwasaidia vijana dhidi ya tatizo la ajira ili wengi waweze kumudu
gharama za maisha.”
Lakini
katika waraka wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Mahanga
alimkosoa Rais Magufuli akisema ameongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri
baada ya kuteua makatibu wakuu 27 wakati anawaaminisha wananchi kwamba
wizara ni 15 tu.
Dk
Magufuli ameunda baraza lenye mawaziri 15, na manaibu waziri 19 na
hivyo kufanya baraza lake kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na
baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 55. Uamuzi wa kupunguza idadi
ya wizara ulikumbana na changamoto ya nafasi za makatibu, ambao hata
hivyo baadhi amewarudisha wizarani ambako watapangiwa kazi na kubakiwa
na makatibu 27.
“Si
kweli kwamba kapunguza ukubwa wa Serikali, bali kaongeza ukubwa wake.
Sina hakika kama wasaidizi wa Rais wamemshauri na kumweleza kwamba
wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema
Dk Mahanga akifafanua kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa wizara na
afisa masuhuli.
Alisema
katibu mkuu ndiye mwenye dhamana ya utendaji na ndiyo maana hata katika
ngazi ya kata, ofisi inaitwa ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na si
ofisi ya diwani.
Kwa
maana hiyo, Dk Mahanga, ambaye kitaaluma ni mhasibu, alisema Rais
alipounda Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambazo awali zilikuwa mbili
tofauti na kuteua makatibu wakuu watatu, kiuhalisia hakuunganisha
wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali.
“Ongezeko
la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha na
kuongeza katibu mkuu mmoja. Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge
mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki tano tu
juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama nyingine ndogo za gari, pia
mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva,” alisema Dk
Mahanga.
Alisema
kwa ujumla ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni kwamba
ataunda Serikali ndogo, hakuitimiza badala yake ameongeza ukubwa wa
Serikali.
Wakati
wa kampeni na alipoapishwa, Rais Magufuli alisema ataunda baraza dogo
la mawaziri, hiyo ilijenga shauku kwa wananchi kufahamu kiwango cha
ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza yaliyoundwa na
watangulizi wake, tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.
Dk Magufuli pia alitoa ahadi hiyo alipozindua Bunge Novemba mwaka jana mjini Dodoma. CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment