MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga ameliagiza Jeshi la Polisi
kuwakamata na kuwahoji Mtendaji wa kijiji cha Kimandaguli na wa kata ya
Lyabukande, kwa kushindwa kuzuia kutoroshwa kwa mwanafunzi aliyefaulu
kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza.
Aidha, ameagiza kukamatwa kwa watu wengine waliowezesha kutoroshwa
kwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14, kutoka katika kijiji cha
Kimandaguli na kata ya Lyabukande vilivyo katika halmashauri ya wilaya
ya Shinyanga.
Agizo hilo limekuja baada ya Mkurugenzi John Myola wa Asasi isiyo ya
Serikali ya Agape, inayojishughulisha na upingaji wa mimba za utotoni
mkoani hapa, kutoa taarifa ya kutoroshwa mwanafunzi huyo kwenye kikao
cha wadau wa elimu kilichofanyika jana.
“Jeshi la Polisi lisimamie kesi ya yule aliyetorosha mtoto wa miaka
13 huko wilayani Kishapu na kukimbilia mkoani Tabora, tunachotaka mkoa
uwaondoe wanaowapa wanafunzi mimba, kuwaozesha au kutorosha wenye umri
mdogo kwa kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wanaondoka mkoani humu,”Rufunga alisema.
Myola alisema, awali alipata taarifa ya simu ya mzazi wa mtoto huyo,
Pauline Maximillian kuwa mtoto wake aliyekuwa amekwenda kisimani kuchota
maji alichelewa kurudi na kuelezwa na watu baada ya kuanza kumfuatilia
kuwa alikuwa amechukuliwa na vijana wawili.
Alisema kuwa, baada ya kupewa taarifa hiyo alimshauri mzazi huyo
akatoe taarifa kwenye uongozi wa Kata, Kijiji na Polisi, na kwamba
pamoja na kufanya hivyo hakufanikiwa kumpata mtoto wake hadi leo kwa
sababu hakupewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi hao wa Kata
na Kijiji. Myola alisema, “Mimi ni shahidi kwa sababu niliongea nao wote
kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo ili walifuatilie na kuhakikisha
mtoto huyo anapatikana, lakini hilo halikufanyika na mzazi hakupewa
ushirikiano unaotakiwa huku taarifa zikisambaa kwamba alitoroshwa na
vijana wawili wa kijiji cha jirani”.
Alisema, mwanafunzi huyo alitoroshwa kabla ya matokeo wakati mzazi
wake anataka apatikane ili aende shule, kwa kuwa amefaulu kujiunga na
kidato cha kwanza. Inaelezwa kuwa mwanafunzi huyo alichaguliwa kujiunga
na shule ya sekondari Lyabukande ambako alipaswa kuwa ameripoti kuanza
masomo tangu Januari 11.
Kuhusu kesi ya watuhumiwa wa kumuozesha mtoto wa miaka 13, wilayani
Kishapu, Myola alisema, Polisi inatuhumiwa kubadili jina na maelezo ya
mtuhumiwa aliyetoroka naye huku tayari asasi hiyo ikiwa na rekodi nzima
ya maelezo ya kwanza yaliyotolewa siku aliyokamatwa.

0 comments:
Post a Comment