SERIKALI imesema kuanzia sasa itatoa mshahara unaolingana kwa
madaktari wote wenye viwango vya taaluma vinavyolingana katika hospitali
zake za rufaa na mikoa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu, alisema hayo jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja
jijini Mwanza, ambapo alizindua duka la dawa la Serikali katika
Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, lililofunguliwa na Bohari Kuu ya Dawa
(MSD).
Ummy alisema, madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za rufaa na
za mikoa za Serikali na ambao wana kiwango sawa cha taaluma lazima
walipwe mishahara inayolingana.
Alisema, lengo la hatua hiyo ni kuwezesha madaktari hao kufanya kazi
kwa usawa pasipo manung’uniko, hivyo kuboresha utoaji huduma za tiba
nchini.
“Tayari nimeishawaelekeza wenzangu pale wizarani wahakikishe kuwa
madaktari wote walio na viwango sawa vya taaluma katika hospitali za
rufaa za serikali na za mikoa,” alisema.
Alisema, haiwezekani daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
alipwe mshahara mkubwa kuliko wa Hospitali ya Sekou Toure ya Mwanza,
wakati viwango vyao vya taaluma vinalingana.
Aliongeza kuwa, kwa kufanya hivyo, Serikali inanuwia madaktari wake
kufanya kazi katika mazingira mazuri huku wote wakiwa wameridhika na
kuachana na dhana kwamba madaktari wengine ni bora zaidi. Alisema pia
kuwa Serikali itawapa vifaa vya kisasa.
Kwa maelezo ya Ummy, katika kukabili changamoto za utoaji wa huduma
ya tiba nchini, Serikali itahakikisha kila Mtanzania anajiunga na huduma
za bima ya afya, ili kumuwezesha kupata tiba kwa gharama nafuu.
Alisema, atahakikisha anamaliza changamoto ya uhaba wa dawa kwa vituo
vya afya, zahanati na hospitali za wilaya na mkoa na kwamba atakuwa
tayari kujiuzulu nafasi yake endapo tatizo la uhaba wa dawa
halitakwisha.
Alisema, hatamuonea huruma mtumishi wa umma atakayejihusisha na vitendo vya wizi wa dawa na vifaa tiba.
“Niliahidi kuwa nitawajibika endapo sitatekeleza ahadi zangu ikiwemo
kumaliza tatizo la dawa katika hospitali za Serikali. Ninyi MSD ni
watendaji kazi wangu, hivyo hakikisheni dawa zinapatikana na mtambue
kuwa hicho ndio kipaumbele cha Serikali ya Rais John Magufuli,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema,
lengo la kufunguliwa kwa duka hilo la dawa ni kuongeza mapato ya
hospitali kupitia huduma hiyo ya dawa.

0 comments:
Post a Comment