Friday, January 22, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amewataka wananchi waliobomolewa nyumba zao katika maeneo ya mabondeni na kukaidi kuhama kwa kuendelea kuishi kwenye vifusi, wahame wenyewe kwa hiari kabla ya kuondolewa kwa nguvu na Jeshi la Polisi.

Pamoja na hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeendelea kutoa tahadhari kwa Watanzania katika mikoa mbalimbali ikiwemo mikoa inayopata mvua mara moja na ile inayopata mara mbili kwa mwaka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Sadiki alisema kitendo cha wananchi hao kuendelea kuishi katika maeneo hayo ya bondeni huku mvua zikiendelea kunyesha ni hatari kwa maisha yao na ni sawa na kutaka kujiua.

“Nawataka waondoke wenyewe kwa hiari yao kwani usalama wa maisha yao uko mikononi mwao, kuendelea kuishi katika maeneo yale ni hatari kwao na watoto wao, lakini kama Serikali hatutakaa kimya na kuona wananchi wetu wakihatarisha maisha yao, tutawaondoa kwa nguvu wakikaidi,” alisema.

“Tunatumia Polisi kwa sababu kitendo cha wao kubaki kwenye eneo la hatari kama hilo la bondeni huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha ni sawa na mtu anayetaka kujiua. Kutaka kujiua ni kosa, sasa sisi tutafanya kama vile tumewakuta hawajajiua tutawakamata kwa nguvu na kuwaondoa pale,” alisisitiza.

Gazeti hili lilishuhudia zaidi ya familia 12 zikiwa zimejijengea juu ya vifusi vibanda chakavu vya mabati na kuendelea kuishi katika bonde la Mkwajuni katika eneo ambalo tayari nyumba zilizokuwapo zimebolewa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula alisema pamoja na kwamba mkoani humo mvua zinaendelea kunyesha kwa kasi, hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza isipokuwa uharibifu mdogo wa madaraja, baadhi ya nyumba kuezuliwa mapaa na maji kufurika kwenye mito.

Akizungumzia utabiri wa hali ya hewa katika kipindi hiki, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi, alisema tayari mamlaka hiyo ilishafafanua kuwa katika maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka, yataendelea kupata mvua.

0 comments:

Post a Comment