SERIKALI ya Awamu ya Tano imesema imejipanga katika kuhakikisha
inapambana na tatizo la rushwa kuanzia kwenye chanzo chake ili
kuiwezesha nchi kuondokana na tatizo hilo na kutengeneza mazingira
mazuri ya kibiashara na uwekezaji.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan baada ya kuzindua Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Global Compact,
wenye lengo la kukutanisha sekta binafsi, kampuni kubwa na
wafanyabiashara kwa lengo la kuboresha na kuimarisha biashara nchini.
Kupitia mtandao huo, sasa sekta binafsi inatakiwa kutekeleza majukumu
yake kwa kuzingatia misingi 10 ya mtandao huo ambayo ni kufanya
biashara kwa kuzingatia haki za binadamu, kupambana na rushwa, kukuza
ajira, kutunza mazingira na kuepuka kutumikisha watoto.
Misingi mingine ni kuepuka utumikishwaji wa ajira wa aina yoyote,
kuzingatia uhuru wa mfanyabiashara na kampuni husika, kuepuka
unyanyasaji, biashara kuzingatia utunzaji wa mazingira, kuhamasisha juu
ya utunzaji wa mazingira na biashara kuepuka mazingira ya rushwa na
hongo.
Makamu wa Rais alisema kupitia mtandao huo, jamii ya wafanyabiashara
inatakiwa kushiriki bega kwa bega katika mapambano dhidi ya rushwa
ikiwamo kushiriki katika kutengeneza sheria na sera nzuri
zitakazorahisisha vita dhidi ya tatizo hilo.
Alisema Serikali kupitia Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na
Shirikisho la Wafanyabiashara Tanzania inatambua kuwa ina wajibu wa
kulinda haki za wananchi, ikiwemo za wafanyakazi na waajiri.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Global Compact Tanzania, Patrick Ngowi
alisema mtandao huo ulianzishwa miaka 15 iliyopita na Umoja wa Mataifa
na hadi sasa una wanachama takribani 12,000 katika nchi 162 na Tanzania
kwa sasa takribani kampuni 42 zimejiunga na ina wanachama 9,000.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro
Rodriguez, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
uongozi wa Rais John Magufuli hasa katika kupambana na matatizo ya
rushwa.

0 comments:
Post a Comment