SAKATA la maofisa watatu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi
wa Mazingira (NEMC), waliosimamishwa kazi kwa tuhuma ya kukiuka miiko
yao ya kazi, limechukua sura mpya, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, kuagiza
wafikishwe mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Pamoja na hayo, Waziri huyo amemsimamisha kazi aliyekuwa mwanasheria wa baraza hilo, John Mnyele kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Akizungumza jana, alisema tayari
amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, kuwasilisha mashtaka
yanayowakabili maofisa hao watatu Takukuru kwa ajili ya uchunguzi na
hatua zaidi, ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Maofisa waliosimamishwa kazi kutokana na udhaifu huo ni pamoja na
Ofisa Mazingira Mwandamizi Dk Eladius Makene, Mwanasheria Daraja la II
Wakili Heche Suguta Manchare ; na Ofisa Mazingira Boniface Benedict
Kyaruzi. Wanatuhumiwa kukiuka miiko ya kazi yao katika kusimamia kiwanda
cha kusindika minofu ya punda kilichopo mkoani Dodoma.
Pamoja na maofisa hao, pia Mwanasheria Mnyele, anayetuhumiwa kuingia
mkataba na Mchungaji Getrude Rwakatare wa kuondoa kesi mahakamani kwa
niaba ya NEMC bila kuijulisha ofisi, naye anachunguzwa na taasisi hiyo
ya rushwa.
Mama Rwakatare kwa sasa ana kesi mahakamani dhidi ya baraza hilo ya
kupinga kubomolewa kwa nyumba yake, inayodaiwa kujengwa mahali
pasiporuhusiwa.
Kiwanda hicho cha minofu ya Punda cha China, kilianza kazi hiyo rasmi
mwaka 2012 huko Dodoma ambapo pamoja na kuchinja, pia huuza nyama hiyo
nje ya nchi, hususan China.
Kiwanda hicho kilipatiwa vibali vyote, ikiwemo cha Mamlaka ya Ukanda
Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) na cha Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi cha kuchinjia.
Pia, kilikuwa na vibali vingine vya Manispaa. Hata hivyo, hakikuwa na kibali cha masuala ya mazingira kutoka NEMC.
Katika ukaguzi uliofanywa siku za nyuma na Baraza hilo, ilibainika
kuwa kiwanda hicho hakina kibali hicho cha mazingira, lakini pia
kilikuwa kikilalamikiwa na wananchi wanaokizunguka kutokana na kutofuata
taratibu za utunzaji wa mazingira.
NEMC ilibaini kuwa kiwanda hicho, hakikuwa na mfumo wa majitaka,
lakini pia kilikuwa kikichoma mabaki yanayotumika kuchinjia ndani ya
kiwanda hicho na moshi wake kusambaa maeneo yanayokizunguka.
Kutokana na makosa hayo, baraza hilo lilikifungia kiwanda hicho kama adhabu na kukilipisha faini ya Sh milioni 240.
Juzi Waziri January pamoja na kuwasimamisha maofisa hao watatu kwa
kukiuka miiko yao ya kazi, pia aliagiza Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo,
Mhandisi Bonaventura Baya, apewe barua ya onyo kali na la mwisho kwa
tuhuma za udhaifu katika usimamizi wa watumishi wa baraza hilo, hivyo
kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa baraza hilo.

0 comments:
Post a Comment