Tuesday, January 26, 2016




RAIS John Magufuli amekataa na kusitisha uhaulishaji wa ardhi ya kijiji cha Mlilingwa, tarafa ya Ngerengere wilayani Morogoro yenye ukubwa wa ekari 3,502.

Ardhi hiyo ilitolewa kwa mwekezaji Oxford Development Limited na hatua hiyo inatokana na kubaini kuwepo kwa mianya ya udanganyifu wakati wa mchakato.

Kutokana na udanganyifu huo, Rais ameamuru kurejesha ardhi hiyo kwa wananchi ili itumike kwa manufaa ya wanakijiji wote.

Mgogoro wa ardhi kati ya wanakijiji cha Mlilingwa na mwekezaji huyo ulimlazimu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kufika kijijini hapo ili kuhakikisha mchakato wa umilikishaji kama ulifuata taratibu .

Akizungumza na wananchi kijijini hapo, alisema baada ya Rais kupitia muhtasari wa kikao kilichofanyika cha kumpa mwekezaji Oxford Development Ltd shamba hilo aligundua ulifanyika udanganyifu mkubwa uliofanywa na viongozi wa vijiji, wilaya na idara ya ardhi na kuamuru shamba lirudishwe kwa wananchi.

Aliwaagiza viongozi wa kijiji cha Mlilingwa, kuchukua hatua kwa waliohusika kumpa mwekezaji shamba la ekari 3,502 kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola kutokana udanganyifu huo.

Pamoja na kutoa agizo kwa Serikali ya Kijiji, pia aliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata viongozi wote, mwekezaji wa shamba hilo na waliohusika kughushi nyaraka hata kama viongozi wameshastaafu.

Alisema hatua hiyo ni kuwezesha watu hao kuhojiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kudanganya serikali iwe fundisho kwa wengine wanaofanya hivyo. Waziri alisema ametumwa na Rais kutumbua jipu hilo alilolikuta mezani mwake, hivyo wote waliohusika ni budi wakamatwe na kuhojiwa na mwishowe wapelekwe mahakamani.

“Nimeagizwa na Rais kuja kutumbua jipu hili na wote waliohusika wakamatwe na wale wanaofanya udanyifu kama huu mwisho wao umefika sasa,” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hivi sasa hakuna mkutano wowote wa kijiji ambao utakaa na kumpitisha mwekezaji kupata shamba bila kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya, ambaye ndiye atakayepeleka barua ya maombi ya mwekezaji kwake ikiwa na muhtasari wa kikao na saini halali za wananchi ndipo akijiridhisha atapeleka ombi hilo kwa Rais.

Katika mkutano huo, kampuni ya Oxford Development Limited iliwakilishwa na Kashoka Panga ambapo baada ya kujiridhisha kuwa utaratibu ulikiukwa, waziri akatoa maagizo hayo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba, alisema serikali ya sasa imepania kufanya kazi kwa vitendo zaidi na hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono kwani matatizo mengi yatafanyiwa kazi.

0 comments:

Post a Comment