Posted by Williammalecela.com on Wednesday, January 13, 2016
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ameamua
kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya kesi ya uchochezi inayomkabili
mwanaharakati wa Kiislamu Shehe Ponda Issa Ponda.
Mwanasheria Mwandamizi katika ofisi ya
DPP, Bernard Kongola amesema kuwa Serikali inapinga kuachiwa kwa Shehe
Ponda ambaye alishitakiwa kwa makosa ya uchochezi katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Morogoro.
“Tayari tumeomba tupatiwe nakala ya
hukumu pamoja na nyaraka za mwenendo wa shauri hilo ili upande wa
mashitaka tuweze kuandaa rufaa yetu Mahakama Kuu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, tangu
waombe kupatiwa nakala ya hukumu hiyo katika mahakama hiyo ya hakimu
mkazi, hakimu ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo bado hajawapatia
upande wa mashitaka hukumu ambayo imechapwa.
“Hatujui kuna tatizo gani, maana
tunapoomba kupatiwa nakala ya hukumu, hakimu amekuwa anatuambia kwamba
bado hawajamaliza kuichapa, kwa kweli hii inashangaza,” alisema.
Novemba 30 mwaka uliopita, Hakimu Mkazi
wa Mahakama ya Morogoro, Mary Moyo alimwachia huru Shehe Ponda kwa
maelezo kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha pasi shaka
yoyote mashitaka dhidi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
0 comments:
Post a Comment