MWENYEKITI wa Chadema mkoa wa Rukwa, Zeno Nkoswe amepongeza Serikali
ya Awamu ya Tano kwa kutumbua majipu na vijipu. Akizungumza katika
mahojiano na gazeti hili, Nkoswe alisema ni jambo ambalo ni jema kwa
serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kuonesha mapema kwamba haina
utani dhidi ya vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za
umma.
Nkoswe ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Chama Cha
Mapinduzi Mkoa wa Rukwa kwa miongo miwili; 1977 hadi 1987 alijiunga
Chadema mwaka 2010 baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM.
“Binafsi nimefurahishwa sana na hatua za serikali hii kwa sababu uozo
ambao tumekuwa tukiupigia kelele, si viongozi wa upinzani bali pia
wananchi wa kawaida, ni haya ambayo sasa tunayaona na kuyasikia,”
alisema Nkoswe.
Aliongeza: “Kazi hii anayoifanya Rais ni ngumu na nzito na kama
anavyosema mwenyewe Rais, tumwombee. Tumwombee kwani endapo atafanikiwa
katika hili, nchi yetu, mbali na kuwa na maendeleo lakini pia itakuwa ya
heshima duniani.”
Alisema ameguswa na kitendo cha makatibu wakuu na manaibu wao kula
kiapo cha maadili hadharani akisisitiza kuwa kiapo hicho ni sawa na
Azimio la Arusha, lingine lililosifika kwa kusimamia madhubuti maadili
ya uongozi.
“Hatua hii ya Rais wetu Magufuli kupambana na kuanika uozo wote
naweza kumfananisha na Hayati Edward Sokoine. Pia zinafanana na hatua za
mwanzo alizochukua Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere dhidi
ya viongozi waliokuwa wakijilimbikizia mali na kuwakoga wananchi mara tu
baada ya Uhuru,” alisema.
Hata hivyo, aliitaka serikali kuwaanika hadharani waliohusika na
kashfa za Richmond, Meremeta, rada, EPA na zote zilizojiri huko nyuma.
Alihimiza Watanzania kujenga tabia ya uwajibikaji kwa kufanya kazi kwa
kujituma bila kusubiri kusukumwa, uaminifu na kutanguliza mbele
uadilifu.

0 comments:
Post a Comment