Thursday, January 28, 2016




MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM), ametaka kuharakishwe kuundwa kwa Mahakama ya Mafisadi na pia kupunguzwa kwa majimbo ya uchaguzi, kwani wabunge wamekuwa wengi bungeni.

Akichangia mjadala wa hotuba ya Rais juzi bungeni mjini hapa, Kessy alitaka pia mbio za Mwenge wa Uhuru zifutwe kwa maelezo kuwa zimekuwa zikiigharimu Serikali fedha nyingi.

“Majimbo yamekuwa mengi, wabunge nao ni wengi hali inayofanya Serikali kutumia fedha nyingi kuendesha Bunge,” alisema mbunge huyo huku akipendekeza vikao vya bajeti vyote vifanyike wilayani ili kupunguza matumizi ya fedha za Serikali, kwa maelezo kuwa watumishi wamekuwa wakijazana Dar es Salaam kutoka mikoa mbalimbali na kulipwa posho kwa ajili ya kwenda kuandaa bajeti.

Alipendekeza pia kuwa kuanzia sasa bajeti ifanyike wilayani kwa mitandao tu, kwa kuwa inatosha. Alizungumzia pia sherehe na kusema kuwa zinafanyika za gharama kubwa kama ilivyo kwa nchi za Kiarabu.

Kadhalika, Kessy alitaka kuangaliwa kwa suala la watumishi wa huduma za meli kwakuwa hawana likizo wala bima, huku mishahara yao ikiwa duni na wanapostaafu hawapewi chochote. Mbali na hayo, Mbunge huyo alitaka apewe kibali cha kufanya ukaguzi nyumba kwa nyumba akieleza kuwa mbolea nyingi imekuwa haifiki kwa wakulima.

“Simwamini Mkuu wa Wilaya, Kamanda wa Polisi wala nani. Mwigulu (Nchemba – Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi) nipe kibali nikakague kijiji kwa kijiji kama mbolea inafika kwa wakulima,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM) alimfananisha Rais John Magufuli kama Yohana Mbatizaji kutokana na kazi anazoendelea kutenda. Huku akinukuu kitabu cha Biblia, alisema Rais amejitoa kutumikia Watanzania sambamba na kuwawajibisha viongozi wanaotumia vibaya madaraka na mali za umma.

Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe (CCM) aliwataka wanasiasa kuacha kuwatisha Watanzania kwa kuingiza maneno ya jazba juu ya hali ya kisiasa ya Zanzibar kuwa hapakaliki ilhali si kweli.

0 comments:

Post a Comment