OFISI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imeingia
katika kashfa nzito na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais Dk. John Magufuli inapambana na kudhibiti matumizi makubwa pamoja
na vita dhidi ya ufisadi.
Ofisi hiyo ambayo inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali
(CAG), Profesa Juma Assad, imethibitika kufanya matumizi hayo pamoja na
matumizi mabaya ya madaraka.
MTANZANIA limebaini katika uchunguzi wake kuwa tangu Profesa Assad
alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na kuapishwa Desemba 2
mwaka huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ofisi hiyo imebariki mambo
kadhaa kinyume na maadili na majukumu yake.
UKARABATIWA NYUMBA
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MTANZANIA inazo, Aprili mwaka jana Ofisi
ya CAG ilianza mchakato wa kukarabati nyumba ya Serikali Plot namba 973
iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam inayotumiwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali.
Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa mujibu wa
taratibu, nyumba zote za Serikali zipo chini ya Wakala wa Majengo ya
Serikali (TBA) na taratibu zote za ukarabati hufanywa na kusimamiwa na
wakala huyo.
“Lakini hapa kwetu hali ilikuwa tofauti kabisa, ofisi ya CAG iliamua
kufanya yenyewe ukarabati huku ikijua kabisa inakiuka utaratibu na
ikatoa kazi hiyo kwa kampuni bila hata kutangaza zabuni, hata kampuni
husika haikuwa na mkataba wowote na ofisi ya CAG.
“Cha kushangaza zaidi kampuni hiyo ya M/SAfriq-Engineering and
Construction Co. Ltd si ya kigeni, ni ya Waswahili wenzetu, lakini
ililipwa gharama za kazi kwa dola za Marekani badala ya shilingi ya
Tanzania.
“Na si kwamba ililipwa kwa wamu kama ilivyo kawaida, bali wao
walilipwa jumla ya dola za Marekani 102,570 kwa mkupuo, tena hata kabla
ya kuanza kazi, ambapo pamoja na gharama zikiwamo kodi za Serikali,
jumla ilifika Sh milioni 281.8,” kilisema chanzo chetu.
Mtaalamu mmoja wa majengo katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es
Salaam (jina tunalihifadhi), ameliambia MTANZANIA kuwa kiasi hicho cha
fedha kinatosha kujenga nyumba nzuri ya kisasa ambayo inaweza kutumiwa
na ofisa yoyote mwandamizi wa Serikali.
Kabla ya Profesa Assad kuingia katika nyumba hiyo, ilikuwa ikitumiwa na CAG aliyestaafu, Ludovick Utouh.
UNUNUZI SAMANI ZA NDANI
Pamoja na hali hiyo ofisi hiyo ya CAG ilikiuka sheria na taratibu za
Serikali kutokana na kiongozi wa taasisi hiyo ya umma kulipwa posho ya
Sh milioni 18 kwa ajili ya kununua samani za ndani ambazo hubadilishwa
kila baada ya miaka mitano.
Katika kutekeleza stahiki yake hiyo, Profesa Assad alikwenda mwenyewe
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kwa ajili ya kununua samani hizo za
ndani Desemba 27, mwaka juzi.
Inadaiwa katika safari hiyo CAG alikiuka sheria na taratibu za
Serikali kwa kutumia zaidi ya Sh milioni 18, ambazo zinaruhusiwa kwa
“KUNDI A” la viongozi kwa mujibu wa waraka wa Idara Kuu ya Utumishi
(Ofisi ya Rais) namba 1 wa mwaka 2014.
Baada ya kununua samani hizo, ofisi yake ililipa fedha za ziada kiasi
cha Sh milioni saba kwa ajili ya kuzisafirisha, pamoja na dola za
Marekani 4,265 (sawa na shilingi milioni 9) kwa ajili ya kodi, visa na
gharama nyingine za usafiri.
UNUNUZIWA SHANGINGI
Mei 13, 2015 ofisi hiyo ya CAG ilimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) barua yenye kumbukumbu
namba FA.242/305/01 yenye kichwa cha habari; “UNUNUZI WA GARI MOJA KWA
AJILI YA MATUMIZI YA CAG TOYOTA LAND CRUISER GX-V8 200 HIGH.”
Baada ya Mtendaji Mkuu wa GPSA, J. Mwambega kupokea barua ya ombi
hilo, alimjibu kwa barua ya Mei 15, mwaka jana, yenye kumbukumbu Na.
CAD.124/318/01/64.
Sehemu ya barua hiyo ambayo nakala ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara
ya Fedha inasomeka; “Napenda kukujulisha kwamba ombi lako la ununuzi wa
dharura halikubaliki kwa sasa kwa sababu upo utaratibu ulioandaliwa na
Serikali kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi.
“Kwa kuzingatia hilo, nakushauri ulipie gharama za ununuzi wa gari
hilo US $ 84,480.05 kupitia akaunti ya GPSA – UNUNUZI WA MAGARI KWA
PAMOJA yenye Na. 0250095100500 ‘US$ Account’ iliyopo benki ya CRDB Bank
(Plc) Tawi la Vijana, Dar es Salaam.”
Pamoja na maelekezo hayo, ofisi hiyo ya CAG ilikiuka maelekezo ya
Mtendaji Mkuu wa GPSA na kununua gari hilo kwa dharura, ambapo malipo
yalifanyika Mei, 15, 2015.
SAFARI YA SEYCHELLES, CHINA
Septemba 5, mwaka jana maofisa kadhaa akiwamo Profesa Assad
walisafiri kikazi kwenda nchini Seychelles, ambapo Septemba 11,
waliondoka nchini humo na kwenda Dubai, Septemba 12 waliondoka Dubai
kwenda Nanjing (China), Septemba 19, waliondoka Shanghai kwenda Beijing
na Septemba 22, waliondoka Beijing kurejea Dar es Salaam.
Uchunguzi umebaini kuwa ukiacha safari ya Seychelles ambako kulikuwa
na mkutano wa wakaguzi wa hesabu, safari ya China haikuwa na uhusiano na
majukumu ya kiofisi, ambapo tiketi za ndege ziligharimu Sh milioni
26.4.
Mbali ya CAG, ofisa mwingine kutoka ofisi yake, Edwin Rweyemamu, naye
alisafiri kwa mzunguko kama huo, ambapo tiketi yake iligharimu Sh mil
21.7.
Ofisa wa tatu ambaye hakwenda Seychelles, lakini aliambatana na CAG
kwingineko ni Elibariki Lyatuu, ambaye tiketi yake iligharimu Sh milioni
21.4.
Wote walisafiri kwa kutumia daraja la “Business Class” ambapo jumla
ya gharama za tiketi zote tatu ilikuwa Sh mil 69.6, gharama ambazo
zinatajwa kuwa kubwa kulinganisha na gharama halisi za safari kwenda
nchi hizo, gharama ambazo hubadilika kutegemea na msimu wa safari.
Uchunguzi wa MTANZANIA ulibaini fedha hizo zilikopwa kutoka fungu la
fedha za Umoja wa Mataifa (UN) zinazotumika katika shughuli mbalimbali
ya ukaguzi wa hesabu, ambapo ofisi ya uhasibu ilisema katika dokezo.
Dokezo hilo linasomeka; “Lipa Sh 69,659,200 kwa ajili ya tiketi za
safari ya CAG na ujumbe wake nchini Seychelles na China. Fedha hii
ilipwe toka UN, lakini tukumbuke kuirudisha mara tutakapopokea mgawo wa
fedha ujao.”
KAULI YA CAG
MTANZANIA ilipomtafuta Profesa Assad na kufanya mahojiano naye
Alhamisi iliyopita ofisini kwake, alikataa kujadili au kuzitolea
ufafanuzi tuhuma dhidi yake.
“Kwanza unajua ni makosa kuwa na nyaraka za ofisi ya Serikali, sasa
kama ukiandika basi na sisi tutachukua hatua. Pia hayo yote uliyosema
mimi sihusiki, watafute watendaji wakupe majibu,” alisema Profesa Assad.
Pamoja na kutoa majibu hayo, alisema atahakikisha anampata mfanyakazi anayetoa siri za ofisi na kumfukuza kazi mara moja.
Baada ya mwandishi kuagana na CAG na kuondoka, akiwa nje ya ofisi
hizo, ofisa mmoja ambaye alihudhuria mahojiano hayo, alimwita na
kumwomba nakala ya nyaraka husika, ambapo alipewa, lakini hakuna majibu
au maelezo yoyote ambayo yalitoka baada ya hapo.
MAJUKUMU YA CAG
Kwa mujibu wa sheria, majukumu ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha wizi, upotevu na ufujaji wa fedha
na mali za umma unadhibitiwa mapema, kwa kufuata taratibu za uhasibu na
kanuni za fedha.
Majukumu mengine ni kusaidia utendaji wa mara kwa mara kwa kutathmini
taratibu za fedha, ili kuhakikisha kuwa zinafaa kwa wakati uliopo na
zinakidhi makusudi ya kuwapo taratibu hizo.

0 comments:
Post a Comment