Friday, January 15, 2016

Asteria Muhozya  na Rhoda James, Mbeya
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesisitiza kauli yake kwamba tarehe iliyopangwa kati
yake na Mameneja wa Tanesco nchi nzima ya kuhakikisha inawaunganishinia umeme wateja waliolipa kwa kipindi kirefu ikiwemo kukamilisha  matatizo ya  LUKU bado iko palepale.Profesa Muhongo ameyasema hayo  leo wakati wa kikao na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na kuongeza kuwa  tarehe 15 Januari,2016, ndio tarehe ya mwisho ya kukamilisha shughuli hizo nchi nzima.

“Katika hili nasema kweli hakuna mzaha. Hatutanii. Wananchi wamechoka, wanataka umeme. Mtindo wa kuandikiana barua tena haupo. Ukishindwa , unajiondoa mwenyewe”,amesisitiza Prof. Muhongo.
Akijibu hoja za Kandoro kuhusu suala la Makaa ya mawe, amesema atahakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kama chanzo kingine cha kuzalisha umeme nchini.
“Mkuu wa Mkoa hili lazima tulishughulikie. Hatuwezi kuacha makaa ya mawe yakae tu kama mapambo wakati tunahitaji sana nishati ya umeme kwa ajili ya kuondoa matatizo ya umeme tuliyonayo”.
Prof. Muhongo ameongeza kuwa, tayari amewaagiza wawekezaji wote wa makaa ya mawe wenye leseni kukutana  nae katika ziara  ili kukubaliana kuhusu suala hilo.” Tayari nimewaambia wote tukutane huku huku site wanieleze wanafanya nini”, ameongeza.
Akieleza kuhusu suala la matatizo ya maji katika vyanzo vya uzalishaji umeme, Prof. Muhongo ameiagiza Tanesco Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuhakikisha wanaandaa  kikao cha wakuu wa mikoa ya Njombe, Iringa, Morogoro na Mbeya ili kufanya tathmini ya utumiaji maji bila kuathiri pande zote ikiwemo kutumika kwa ajili ya umeme na kilimo.
“Najua maji yanahitajika sana katika kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji ambacho ndio cha kisasa. Lakini hata nishati inahitaji maji. Nawaomba kutaneni zungumzeni halaf tembeleeni maeneo ya mabonde na mashamba mpate data zote,  mkimaliza tuangalie suala la kisera linasemaje .  Suala hili ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya uzalishaji nishati na kilimo. Lakini pia tunahitaji kuwa na tamko la pamoja,” amesema Prof. Muhongo.
Aidha, Prof Muhongo ameagiza kuwa katika kikao hicho kiwakutanishe pia na Wakuu wa mabonde ili suala hilo liweze kujadiliwa na pande zote.
“Mkuu wa Mkoa nashauri na wakuu wa mabonde wawepo. Lakini pia wanatakiwa kuangalia suala la utoaji vibali kwa sababu kuna umwagiliaji mwingine sio mzuri”. Wazalishaji wadogo wanalia sana na suala la uharibifu wa vyanzo vya maji. Nimepita maeneo mengi wengi wanalia na wana hofu na maji. Wale wanatusaidia sana kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme. Kwetu sisi  wazalishaji wadogo ni muhimu sana”, amesema Waziri Muhongo.
Awali Mkuu wa Mkoa alimweleza Prof. Muhongo kuhusu suala la Makaa ya mawe ya Kiwira na kumweleza umuhimu wa kuendeleza miradi hiyo kwa maendeleo ya nchi na katika kusaidia taifa kuwa na kiasi cha umeme wa kutosha.
” Prof. nashauri sana  wizara yako ifufue  mgodi wa Kiwira kutokana na umuhimu wake kwa taifa.” Awali mgodi huu ulikuwa  unasaidia kuingiza umeme kwenye gridi hii ni muhimu. Mkoa wetu umebarikiwa kuwa na madini na ni wa tatu katika kuchangia pato la Taifa. Tukiongeza na Kiwira taifa litanufaika zaidi,” ameongeza Kandoro.
Akiwa mkoani Mbeya Prof. Muhongo atatembelea mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira, Wachimbaji wadogo wa madini Chunya, maeneo yenye viashiria vya nishati ya jotoardhi Mbaka, Bonde la mto Songwe kwenye mradi wa kuzalisha umeme na maeneo mengine.

0 comments:

Post a Comment