WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameagiza
mameneja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), watakaoshindwa kutekeleza
maagizo ya wizara hiyo, waondolewe kazini ifikapo Machi mosi mwaka huu.
Alisema hayo jana wakati wa kikao chake na watendaji wa Tanesco na
taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofanyika katika
kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni kuunganisha huduma kwa
wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya ankara za umeme, kupunguza
manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa
mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, ifikapo Machi mosi mwaka huu
atatuthibitishia kama mameneja hawa wataendelea na majukumu haya
wanayosimamia ama la, na hii itatokana na ufanisi wa utendaji katika
majukumu tuliyowapangia,” alisema Profesa Muhongo.
Mbali na mameneja hao, Profesa Muhongo ameagiza Kitengo cha Uwekezaji
cha Tanesco, kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo Aprili 2
mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo waondolewe katika nafasi hiyo kwa
kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni makubwa na tuna miradi
mingi ya usambazaji umeme kwa wananchi ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa
Umeme Vijijini). “Wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na
kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi mipya ya umeme, tutashindwa
kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha umeme tulichokuwa
nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.

0 comments:
Post a Comment