MAMLUKI waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), siku zao
zinahesabika, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais mstaafu wa Awamu
ya Nne, Jakaya Kikwete, kumuagiza Makamu Mwenyekiti, Tanzania Bara,
Philip Mangula kuanza kuwashughulikia.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya 39 ya kuzaliwa kwa chama hicho
yaliyofanyika jana katika Uwanja wa Namfua, mkoani Singida, Kikwete
alisema chama hicho kimevuka salama katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa
Oktoba mwaka jana, pamoja na baadhi ya wenzao kuondoka.
“Tunashukuru uchaguzi ulipita na Chama kimevuka salama katika
mchakato mzito kinyume na watu walivyotutabiria kifo... haukuwa rahisi
kwetu kwa sababu ulizidiwa na kelele na vitisho pamoja na kuwepo wenzetu
waliotuhama na kudhani tutakufa lakini hatukutetereka. “Tunajua wako
wengine waliobaki kama mamluki, lakini wajue siku zao zinahesabika maana
hatutakubali kuendelea kunyonywa damu, natumaini Mangula umeanza
kuwashughulikia hawa mamluki,” alisema Mwenyekiti huyo anayemaliza muda
wake.

0 comments:
Post a Comment