Polisi walichapa usingizi, waziri aagiza uchunguzi
NI umafia wa aina yake uliofanikisha watuhumiwa watatu, wakiwamo wa
ujangili na mauaji kutoroka kwa kutoboa tundu kwenye ukuta wa Kituo cha
Polisi Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Watuhumiwa hao, wawili wa ujangili na mmoja wa mauaji, walitoroka
muda mchache baada ya kutoka mahakamani ambako walipelekwa kutokana na
kesi zilizokuwa zinawakabili.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Februari 19, mwaka huu saa nane
usiku, ambapo inaelezwa kuwa watuhumiwa hao walitoroka wakati mvua
ikinyesha baada ya kutoboa ukuta na kitu chenye ncha kali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bariadi, Kaimu Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Audax Majaliwa, alisema kutokana na tukio hilo
askari saba wanashikiliwa.
Alisema watuhumiwa hao kabla ya kutenda tukio hilo, Februari Mosi
mwaka huu, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya
Meatu kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazowakabili.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema baada ya kusikilizwa kwa kesi zao,
walirudishwa mahabusu katika kituo hicho cha polisi, wakisubiri
kukamilika kwa taratibu za kuhamishiwa katika gereza la wilaya.
Aliwataja watuhumiwa hao waliotoroka kuwa ni pamoja na Chiluli Sitta
(28) mkazi wa kijiji cha Mwasangula Kata ya Itinje wilayani humo, ambaye
alikuwa akikabiliwa na kesi a mauaji.
Wengine ni Msanja Ndangule (45) na mtoto wake Paschal Masanja, wote
wakazi wa Kijiji cha Sapa, Kata ya Itinje wilayani humo ambao walikuwa
wakikabiliwa na kesi ya ujangili.
“ Watuhumiwa hawa walitumia sehemu ya bafu na choo ambayo kwa kawaida
inakuwa imeharibika au kuloana sana kutokana na mkojo ambao ukojelewa
na mahabusu.
“Kwa kawaida mkojo na simenti havipatani, tuna hofu kuwa sehemu hiyo
ilikuwa haina ugumu hata kidogo,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.
Alisema kuwa pamoja na ukuta huo kuonekana umeharibiwa na mkojo hivyo
kuwarahisishia watuhumiwa hao kutoboa na kutoroka, kulikuwa na uzembe
uliofanywa na askari waliokuwa zamu pamoja na mkuu wa kituo hicho.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema katika mahabusu hiyo walikuwamo
watuhumiwa sita, ambapo watatu walitoroka na wengine wawili walibaki,
ambao ndiyo walitoa taarifa kwa askari kuwa wenzao wametoroka kwa
kutoboa ukuta.
“Jambo la kushangaza kwanini wengine walibaki? Na hawa waliotoroka
wanatoka kata moja, tuna hofu hapa kuwa kulikuwepo na njama, lakini kwa
waliobaki walieleza kuwa waliona dalili mapema kwa wenzao kuwa wako
kwenye mipango mikubwa,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.
Majaliwa alisema kuwa kutokana na tukio hilo tayari jeshi hilo
limeanza kuchukua hatua za haraka, ambapo mpaka sasa askari saba
wanashikiliwa ili kusaidia uchunguzi.
Aliwataja askari hao kuwa ni G. 8371 PC Adam, F. 9840 DC Hussen, D.
5582 Koplo Peter ambaye alikuwa kiongozi wa zamu siku ya tukio, G. 4806
PC John, G.8602 PC Yassin, H. 8410 PC Hery na WP. 1125 Hadija.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema kuwa baada ya hatua hizo kwa askari
hao, taratibu nyingine za kushtakiwa kijeshi zitaendelea mara baada ya
uchunguzi kukamilika.
Alisema kuwa askari hao wanahusika moja kwa moja kwani licha ya mvua
kunyesha, walitakiwa kufanya kazi ya kulinda kituo hicho pamoja na
watuhumiwa hao, na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha walikuwa
wamelala.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema hadi sasa watuhumiwa hao
hawajapatikana na msako mkali unaendelea wa kuwatafuta ili kurudishwa
gerezani kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashtaka yanayowakabili.
WAZIRI KITWANGA
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga,
amesema ametuma timu ya uchunguzi wilayani Meatu ili kubaini chanzo cha
watuhumiwa hao kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
“Nawaomba muwe na subira, nimetuma timu ya wataalamu wangu kwenda
kuchunguza kwa kina sababu za watuhumiwa hawa kutoroka wakiwa chini ya
ulinzi…nitaujulisha umma baada ya kupokea ripoti.
“Naamini ripoti itakayokuja ndiyo itanipa picha halisi ya tukio hili,
maana najiuliza ilikuwaje watu watoroke wakati wanakabiliwa na makosa
mazito hivi,” alisema Waziri Kitwanga.
Alisema kutokana na hali hiyo, ametuma kikosi maalumu cha makachero kwa ajili ya kuwasaka kwa udi na uvumba watuhumiwa wote.

0 comments:
Post a Comment