Baadhi ya magari ya wateja yakiendelea kuoshwa katika kampuni ya Shine Eco Wash Limited yenye makazi yake Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wafanyakazi katika kampuni ya Shine Eco Wash Limited yenye makazi yake Mlimani City jijini Dar es Salaam akiendelea na kazi ya uoshaji.
Kazi ya uoshaji wa magari ikiendelea katika kampuni hiyo
Na Greyson Mwase
Kampuni inayojishughulisha na uoshaji wa magari kwa njia ya mvuke imeanza kutoa huduma zake jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalum Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Elia Richard Moshi alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kutoa huduma ya kipekee kwa kuosha magari kwa kutumia mvuke ni kuzuia uharibifu wa mazingira.
Akielezea utofauti wa huduma hiyo na huduma zingine Moshi alisema kuwa kampuni inatumia maji yasiyo na kemikali ya aina yoyote (distilled water) ambapo gari moja huoshwa kwa kutumia lita tatu hadi tano za maji kwa njia ya mvuke ijulikanayo kama steaming.
Alisema kuwa awali alifanya utafiti na kubaini kuwa kwa kawaida gari moja huoshwa kwa kutumia lita 85 hadi 125 hali inayochochea upotevu wa maji na uharibifu wa mazingira, hali iliyopelekea yeye kubuni wazo la kuanzisha kampuni ya kuosha magari kwa kutumia maji kidogo yasiyo na kemikali kwa kutumia mashine maaluum.
Aliongeza kuwa huduma nyingine wanazotoa kama kampuni ni pamoja na kung’arisha magari kwa nje (body polishing) ili kuondoa mikwaruzo na madoa sugu, kung’arisha gari kwa ndani (interior polishing) na kusafisha engine bila kutumia maji.
“Unajua unapotumia maji kuosha engine ya gari hususan kwa magari ya kisasa, unaharibu gari, hivyo tunaosha bila kutumia maji kwa kutumia mashine maalum pamoja na kung’arisha,”alifafanua Moshi.
Aliendelea kufafanua kuwa watumiaji wa magari wanashauriwa kuosha magari kwa kutumia mvuke angalau mara moja kwa mwezi na kuwataka wamiliki wote waishio jijini Dar es salaam kupeleka magari yao katika kampuni yake yenye makazi yake katika viwanja vya Mlimani City kwa ajili ya kuoshwa.
Akielezea malengo ya kampuni yake katika kusambaza huduma kwa wafanyakazi waliopo maofisini, Moshi alisema kuwa kampuni ina mashine maalum (mobile machine) zenye uwezo wa kufanya kazi sehemu yoyote ambapo wateja wanaweza kusogezewa huduma kwenye maofisi yao.
“Wateja waliopo maofisini wana uwezo wa kujiorodhesha na sisi kama kampuni kuwafuata maofisini na kuwaoshea magari yao kwenye parking zao huku wakiendelea na shughuli zao kama kawaida na kwa usalama zaidi” alifafanua.
Hata hivyo aliongeza kuwa kampuni ina mpango wa kufungua matawi jijini Dar es Salaam na katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Kilimanjaro na mingine kwa siku za usoni
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa jijini Dar es Salaam kuhusu huduma ya kampuni hiyo walisema kuwa wameanza kunufaika na huduma hiyo na kufurahishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Salum Salehe mkazi wa Masaki jijini Dar es salaam alisema kuwa tangu ameanza kutumia huduma hiyo, gari yake imekuwa ikionekana mpya kila kukicha na kuwataka watumiaji wengine wa magari kutumia kampuni hiyo katika uoshaji wa magari yao.
Alisema kuwa mbali na mwonekano wa gari yake kuimarika, kampuni hiyo imekuwa ikokoa muda mwingi kwani anakabidhi gari kwa kampuni na kuendelea na majukumu yake kama kawaida ambapo hufuata baadaye baada ya kazi ya uoshaji kukamilika.
Naye Victor Moshi mkazi wa Kinondoni aliongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwasiliana na wateja wake kwa njia ya sms kwa ajili ya kuwashauri juu ya utunzaji wa magari yao jambo ambalo ni jema.
0 comments:
Post a Comment