Monday, March 7, 2016


Mke wa rais mama Janeth Magufuli,amekabidhi msaada wa vyakula na vifaa vya kuzalishia umeme wa jua katika kituo cha makazi ya wazee na wasiojiweza cha Kalwande, kilichopo Bukumbi wilayani Misungwi mkoani Mwanza, vilivyotolewa na benki ya CRDB vyenye thamani ya shilingi milioni 53.

Msaada huo uliotolewa katika kituo hicho kinachohudumia zaidi ya watu 100, ni pamoja na tani sita za mchele, tani sita za unga, tani tatu za maharage, mafuta ya kupikia lita 1,000 na kilo 2,500 za sukari. 

Msaada mwingine ni madawa mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 2 pamoja na vifaa vya kuzalishia umeme wa jua, Solar Panel vyenye thamani ya shilingi milioni 16.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB Dk. Charles Kimei, amesema benki yake inatambua changamoto mbalimbali wanazozipata wazee na walemavu wasiojiweza na kuongeza kuwa taifa bora ni taifa ambalo linajali na kutambua mchango wa wazee katika ujenzi wa taifa hilo, kwa hali hiyo amesema ni jukumu la kila mtanzania kuhakikisha kuwa wazee,walemavu na wasiojiweza katika jamii wanapata matunzo stahiki.

Awali akisoma taarifa ya kituo hicho, afisa mfawidhi wa makao ya wazee na wasiojiweza Marco Bundala anaeleza changamoto zilizokuwa zinakikabili kituo hicho, ikiwa ni pamoja na uchakavu wa majengo, kukosekana kwa nishati ya umeme pamoja na kukosekana kwa gari la kubebea wazee pindi wanapohitaji kupelekwa hospitalini.

Miongoni mwa wadau wengine walioguswa na mahitaji ya wazee hao ni pamoja na mfuko wa pensheni wa PPF kanda ya ziwa na Baps Charities ambao ni watanzania wenye asilia ya kiasia waliopo makoroboi jijini Mwanza.

0 comments:

Post a Comment